Yanga: Tutakufa na TP Mazembe

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:09 AM Dec 11 2024
Wachezaji wa Yanga.
Picha:Mtandao
Wachezaji wa Yanga.

HUKU ikitarajia kuelekea DR Congo kesho kutwa, Alhamisi tayari kwa mchezo wao wa Kundi A Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe, Mkurugenzi wa Ufundi wa Klabu ya Yanga, Abduhamid Moallin, amesema kwa sasa wamesahau kila kitu kilichotokea nchini Algeria, badala yake wanaelekeza nguvu kwenye mechi hiyo itakayopigwa Jumamosi katika uwanja wa klabu hiyo mjini Lubumbashi.

Mkurugenzi huyo amewataka wanachama na mashabiki kusahau yaliyopita, badala yake kuisapoti timu ili kwenda kupata ushindi ugenini utakaowarudisha kwenye reli ya kujaribu kucheza robo fainali ya pili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Akizungumza juzi jioni, Moallin, ambaye ana taaluma ya ukocha, alisema kipigo walichokipata cha mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Julai 5, Algiers nchini Algeria, dhidi ya MC Alger, Jumamosi iliyopita, kilichangiwa na vitu mbalimbali, ikiwamo kikosi kukumbwa na majeruhi, pamoja na hali ya hewa.

"Tuna muda mfupi sana wa kujiandaa kwa mazoezi na safari,  lakini tutaanza mazoezi haraka kwa ajili ya mchezo dhidi ya TP Mazembe, mchezo ulikuwa mgumu, tuliweka nguvu zote, wachezaji walicheza kwa juhudi zao zote, lakini vitu vingi vimechangia, hali ya hewa haikuwa rafiki kwetu, kwa sasa tunasahau hilo tunajiandaa na mechi ijayo, ni muhimu sana kwetu kwani inashikilia mustakabali wetu.

"Tunatakiwa tushinde ili kurudi kwenye mstari, hivyo ni lazima tukacheze kama fainali," alisema kocha huyo wa zamani wa KMC na Azam FC.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Alex Ngai, ambaye aliambatana na kikosi hicho, alisema jijini Dar es Salaam kuwa kilichowagharimu ni idadi kubwa ya majeruhi waliokuwa nao, lakini akiahidi kuwa hawajakata tamaa na safari bado inaendelea.

"Ilikuwa ni mechi ngumu, mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kingine kilichotugharimu ni idadi ya majeruhi, tumepoteza kwa mabao 2-0, lakini safari bado inaendelea pamoja na kwamba kundi ni gumu kwani tumepoteza michezo miwili, ila haijaisha mpaka iishe, tunajiandaa siku mbili hizi, tutaelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mchezo wetu wa tatu, bahati nzuri wachezaji wetu wote majeruhi wameshapona, kasoro Shadrack Boka ndiyo hatutakuwa naye katika mchezo ujao," alisema Ngai.

Baada ya kufungwa mabao 2-0 katika michezo miwili mfululizo dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan, Yanga inaburuza mkia kwenye Kundi A ikiwa haina pointi wala bao, TP Mazembe ikiwa na pointi moja kwenye nafasi ya tatu, MC Alger ina pointi nne, ikiwa nafasi ya pili na Al Hilal ikiongoza kundi kwa kukusanya pointi sita hadi sasa.