Yanga kazi moja ushindi

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:53 AM Jan 04 2025
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic.
Picha:Yanga
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic.

MASHAMBULIZI mwanzo mwisho, hayo ni maneno ya wawakilishi wa Tanzania, Yanga kuelekea mechi ya Kundi A ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe kutoka DR Congo itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo Yanga itashuka ikiwa na kazi moja tu ya kuhakikisha inapata ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Timu hizo zilipokutana katika mchezo wa raundi ya tatu uliopigwa kwenye Uwanja wa Mazembe, Mjini Lubumbashi Desemba 14, mwaka jana, zilitoka sare ya bao 1-1.

Akizungumza jijini jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, ameahidi kutowapa 'pumzi' wapinzani wao kwa kufanya mashambulizi kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo huo ili kutimiza malengo.

Ramovic alisema hawajui wapinzani wao watacheza vipi, lakini wamejiandaa kuwadhibiti, kuwabana na kutowapa nafasi ya 'kupumua' kwa kutengeneza nafasi za kufunga muda wote wa mchezo huo.

"Nilipokuja wiki sita zilizopita niliona timu imekosa utimamu wa mwili, lakini ni kama wiki nne sasa, nimeongeza nidhamu ya mazoezi na sasa unaona taratibu timu inarejea. Katika mchezo huu pengine TP Mazembe watacheza aina ile ile ya mipira mirefu na krosi katika boksi, lakini tumejiandaa vizuri na wachezaji wameanza kushikamana kama timu, na hii inanipa sana faraja kama kocha.

Tunahitaji kucheza kwa kasi ya hatari, tunahitaji kutompa mwanya mpinzani wetu wala kupumua, kuna namna tumesogea ila bado hatujafika ninapotaka, mashabiki wajue tunataka kushambulia mpaka mwisho, hatutaki kumpa muda wala nafasi mpinzani wetu kufikiria chochote," Ramovic alisema.

Naye Kocha Mkuu wa TP Mazembe, Lamine Ndiaye, aliliambia gazeti hili matokeo ya sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopita hayakupokewa vizuri na viongozi na mashabiki wa timu hiyo, hivyo wamejizatiti kushinda katika mchezo wa leo.

Ndiaye alisema amefanyia kazi mapungufu aliyoyabaini na amejiandaa kupata matokeo mazuri ya ugenini.

"Natumai kesho (leo), tutacheza vizuri na tutapata matokeo," alisema kocha huyo.

Mchezaji wa timu hiyo, Atibu Radjabu, aliwataka mashabiki wa soka nchini wajitokeze kwa wingi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kushuhudia kandanda safi litakaloonyeshwa.

"Sisi kwetu mpira ni sherehe, wapinzani wetu nadhani wapo tayari kwa mechi na sisi tupo tayari kwa mchezo huu," alisema mchezaji huyo.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye uwanja huo ilikuwa Februari 19, mwaka 2023 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, Yanga ikishinda mabao 3-1, shukrani kwa Kennedy Musonda, Mudathir Yahya na Tuisila Kisinda huku lile la kufutia machozi la TP Mazembe likipachikwa wavuni na Alex Ngonga.

Yanga inashika 'mkia' katika Kundi A ikiwa na pointi moja, huku TP Mazembe yenye pointi mbili ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya MC Alger ya Algeria na vinara Al Hilal ya Sudan yenye pointi tisa.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walianza hatua ya makundi kwa kukubali kufungwa mabao 2-0, nyumbani na Al Hilal na ilipoenda ugenini Algeria ilifungwa tena idadi kama hiyo ya mabao.

Wawakilishi wengine wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa ni Simba ambayo kesho itashuka ugenini Tunisia kucheza dhidi ya CS Sfaxien ya huko.