Wachezaji Simba waahidi ushindi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:55 AM Sep 13 2024
news
Picha: Simba SC
Wachezaji Simba waahidi ushindi

WAKATI kikosi cha Simba kikiwasili jana jijini Tripoli Libya kwa ajili ya mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli Jumapili kwenye Uwanja wa Juni 11, wachezaji wa timu hiyo wamesema wanaanza kucheza michuano ya kimataifa ambayo wanaipenda na kuahidi ushindi kwenye mchezo huo.

Wakizungumza wakiwa Uwanja wa Ndege jijini Istanbul nchini Uturuki jana kabla ya kuunganisha ndege kuelekea Libya,  wachezaji wa timu hiyo wamesema kama kuna wakati huwa wanafurahi, basi ni kushiriki michuano ya kimataifa iwe ya Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho.

Beki mkongwe wa timu hiyo, Shomari Kapombe, amesema kwa vyovyote vile hawawezi kukubali kupoteza mechi hiyo kwani wanataka kuendelea kucheza michuano walioizoea ambayo wanaipenda, michuano ya kimataifa.

 "Hiki ndicho kipindi ambacho wanachama na mashabiki wa Simba wanakipenda kuliko kipindi chochote kile, hiki ni kipindi cha michuano ya kimataifa na hata sisi wachezaji ndiyo wakati ambao tunaupenda sana, kikubwa cha kuwaambia mashabiki wetu kuwa matarajio yetu ni makubwa sana kuna wachezaji wengi wapya wenye ari, nguvu na kujituma na wenye kujitolea, hiki kitu kimekuja kuongeza morali katika kikosi chetu, sasa umefika wakati wa kwenda kufanya kwa vitendo kwa sababu muda wa maandalizi umeisha, niseme tu kuwa kila mchezaji yupo tayari kwa huu mchezo," akisema Kapombe.

Kiungo mshambuliaji mpya wa timu hiyo aliyesajiliwa kutoka KMC, Awesu Awesu, amesema wanachama na mashabiki wa Simba wanapenda sana kuona timu yao ipo kwenye hatua ya makundi Afrika na huwa hawajisikii vizuri kama haipo kwenye hatua hiyo.

"Mimi tangu nipo KMC, nawaona kabisa kuwa mashabiki wa Simba hata kama wasipofanya vyema kwenye ligi, lakini kama wako kwenye hatua za makundi michuano ya kimataifa wanafurahi sana, yaani tunatakiwa kufanya tufanyavyo ili wajisikie wenye furaha, wanaihitaji hatua hii," alisema Awesu.

Kikosi cha Simba kilitua jana hiyo hiyo nchini Libya baada ya kuondoka Uturuki.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kuondoka Istanbul, Meneja wa kikosi hicho, Patrick Rweyemamu, alisema waliondoka na kikosi cha wachezaji 17, viongozi na benchi la ufundi, huku baadhi ya wachezaji wakitarajia kuwakuta nchini humo.

"Tupo makundi mawili, wengine wanatoka kwenye vikosi vya timu za taifa, wao waliunganisha moja kwa moja Libya, sisi hapa tuna wachezaji 17, benchi la ufundi na viongozi," alisema.

Baada ya mechi hiyo, mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa, Septemba 20, Uwanja wa Banjamin Mkapa, Dar es Salaam.