WACHEZAJI wa Kilimanjaro Wonders, wamesema pamoja na kufungwa mabao 6-0 dhidi ya Simba, kwenye mchezo wa Kombe la FA katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam juzi, lakini wamefurahia kuonekana kwenye televisheni nchi nzima, huku wakidai ilikuwa ni moja ya malengo yao ili kuwaonesha watu kuwa wana vipaji vya kusakata kabumbu.
Wachezaji hao, Hamisi Ramadhani, Faraji Rashid, Patrick Sebastin na Khatibu Kigasa, walisema kitendo cha kupangiwa kucheza na Simba, walijua ni fursa ya kwenda kuonesha watu kuwa kuna vipaji vilivyojificha, na kwamba licha ya kufungwa mabao hayo, wameonesha vipaji vyao na wengi wamefurahi.
Faraji, ambaye mashabiki wa soka wamempachika jina la 'Salah', wakimfananisha na mchezaji wa Livepool ya England, Mohamed Salah, amesema amefurahi kuona mashabiki wengi na hata wachezaji wa Simba wamefurahishwa na kiwango chake.
"Nilikuwa nacheza huku nikijua tunaoneshwa kwenye TV, kwa hiyo nilikuwa nafanya vitu ambavyo watu wataviona, nilitaka watu waone kipaji changu ili nionekane, nichukuliwe na mimi niweze kwenda kwenye timu zenye uwezo nipate kipato cha kuniwezesha maisha yangu kuwa mazuri," alisema winga huyo machachari.
Alisema awali alikuwa na wasiwasi kucheza na wachezaji wakubwa kwani ni mara yake ya kwanza kuwaona laivu
"Kitu kipya nilichokutana nacho uwanjani ni presha ya mashabiki, kupokea pasi mbele ya mchezaji mkubwa ambaye huwa unamuona kwenye TV, nayo pia ilikuwa kama nina kigugumizi hivi, lakini baadaye nikazoea," alisema.
Hamisi, alisema alikuwa anacheza ili aonekane kwenye televisheni akionesha uwezo wake, kwani lengo lake anatakamni kucheza kwenye Kituo cha TFF.
"Ndoto yangu kubwa ni kupambania nembo ya timu ya taifa, ukiangalia wana michuano ya CHAN Agosti na AFCON 2027, natamani niwe mmoja wa wachezaji hao, pia kuichezea Simba kwenye Ligi Kuu misimu kadhaa ijayo," alisema mchezaji huyo aliyecheza beki wa kati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED