Stumai, Aisha waingia vita ya Kiatu Ligi Kuu ya Wanawake

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:13 AM May 08 2024
Stumai Abdallah wa JKT Queens (kushoto) na Aisha Mnuka wa Simba Queens ambao wanachuana kuwania  Kiatu cha Mfungaji Bora.
Picha: Nipashe Digital
Stumai Abdallah wa JKT Queens (kushoto) na Aisha Mnuka wa Simba Queens ambao wanachuana kuwania Kiatu cha Mfungaji Bora.

WAKATI Ligi Kuu ya Wanawake nchini ikibakiza raundi nne kabla ya kutamatika huku Simba Queens ikibakiza pointi nne tu kutawazwa mabingwa wapya wa msimu wa 2023/24, vita mpya ya kuwania Kiatu cha Mfungaji Bora, imeibuka.

Mastraika hatari wawili wa Kitanzania, Stumai Abdallah wa JKT Queens na Aisha Mnuka wa Simba Queens wanachuana vikali ili kutwaa Kiatu cha Dhahabu mwishoni mwa msimu wa ligi hiyo.

Licha ya kwamba timu yake inashika nafasi ya pili, Stumai wa JKT Queens anaongoza kwenye upachikaji mabao akiwa ameshacheka na nyavu mara 18, akifuatiwa na Aisha ambaye timu yake, Simba Queens inaongoza msimamo wa ligi hiyo, akiwa na mabao 16.

Aisha amesema amedhamiria kuisaidia timu yake kufikia malengo huku lengo lake la pili likiwa ni kuwa mfungaji bora msimu huu.

"Nikipata nafasi natumia kwa sababu nataka timu yangu ishinde, lakini lengo langu la pili ni kuwa mfungaji bora, mwanzoni malengo yangu yalikuwa kufunga mabao 22, lakini naona natakiwa kuzidisha ili kuwa mfungaji bora," alisema Aisha.

Katika mbio hizo za kuwania ufungaji bora Stumai na Aisha wanafutiwa kwa mbali na Winfrida Gerald ( JKT Queens) ambaye amefunga nane, Asha Djafar na Jentrix Shikangwa (Simba Queens) wakitikisa nyavu mara sita.

Donisia Minja (JKT Queens), Janeth Nyagali (Amani Queens), Hasnath Ubamba (Fountain Gate), Magreth Kunihira (Ceassia Queens) na Nelly Kache (Alliance Girls) kila mmoja amecheka na nyavu mara tano.

Waliofunga mabao manne ni Amina Ramadhan (Fountain Gate), Amina Bilal na Jamila Rajabu (JKT Queens), Janeth Matulanga (Ceassia Queens), Joyce Meshack (Baobab Queens) na Kaeda Wilson (Yanga Princess).

Katika msimamo wa ligi hiyo Simba Queens wanaongoza ligi wakiwa na pointi 40 na JKT Queens ambao ni mabingwa watetezi wapo nafasi ya pili na pointi 31 ambapo kila moja inahitaji kusaka ushindi katika michezo yao iliyosalia ili kufikia malengo.