SERIKALI kupitia kwa msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa imezitakia heri klabu za Simba na Yanga kwenye mechi zao za kimataifa zitakazochezwa mwishoni mwa wiki hii zifanye vizuri ili kusongambele kwenye michuano hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma baada ya makabidhiano ya Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema.
“Mwishoni mwa wiki kutakuwa na michezo ya kimataifa ya klabu ya Yanga na Simba nawatakia heri wafanye vizuri, wapate pointi na kujihakikishia safari ya kusonga mbele kwenye mashindano wanayoshiriki,” alisema Msigwa.
Aidha, alisema kwenye Wizara kuna miradi mikubwa ya AFCON inakuja na kuomba waandishi wasaidie kuitangaza.
“Pia kwa sasa tuiandae nchi kwa ajili ya CHAN na AFCON ni matukio makubwa ambayo Wizara yetu inahusika, tunaomba ushirikiano wenu katika kutangaza,”alisema.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa fainali za Afcon za mwaka 2027 pamoja na Kenya na Uganda na CHAN zitakazofanyika mwakani kwa kushirikiana na nchi za Uganda na Rwanda.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED