HUKU Rais Samia Suluhu Hassan akitoa motisha ya Sh. milioni 700 kwa wachezaji wa Timu ya Soka ya Tanzania (Taifa Stars), kufuatia kufuzu tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025), ni, Serikali imesema imeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo kwa kupambana hadi kufikia malengo ya nchi.
Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Guinea, umeifanya Taifa Stars kufikisha pointi 10 na kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi H nyuma vinara Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), iliyomaliza na pointi 12 kibindoni.
Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA', alisema kilichoonyeshwa na wachezaji wa Stars ni kuipambania bendera ya taifa katika mechi zote za hatua ya makundi.
Mwana FA alisema mara baada ya mechi dhidi ya Ethiopia ambayo alikuwa sehemu ya msafara wa timu hiyo, juzi wachezaji walionyesha zaidi kiu ya kutaka kushiriki fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
"Bahati nzuri hata mchezo wa Guinea na DR Congo bado tulikuwepo Congo, baada ya mchezo ule wachezaji wa Guinea walishangilia sana kuwafunga Congo, nilikuwa na wachezaji wa Stars wakaniambia waache washangilie sisi tutaenda kumalizana nao kwa Mkapa, na kweli leo (juzi), wachezaji wameonyesha kile walichoniambia, wamepambana na Guinea amekufa hapa kwa Mkapa," alisema Mwana FA.
Naibu Waziri huyo alisema Serikali imeridhishwa na juhudi na kujituma kwa wachezaji hao wakati wote na kuwapongeza kutokana na kuthamini mchango wao.
"Tunaenda kujipanga sasa kwa ajili ya kuhakikisha timu inakuwa na maandalizi mazuri kuelekea katika fainali hizo zitakazofanyika Morocco, tumefarijika sana," alisema kiongozi huyo.
Naye Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco', aliliambia gazeti hili amefurahi kuwa sehemu ya historia ya soka la Tanzania kwa kuiwezesha Taifa Stars kufuzu kwa mara ya nne kucheza fainali za AFCON.
"Najua hatukupewa nafasi kubwa ya kufuzu, lakini nilijua nafasi ipo kama tutapambana na kuchanga karata zetu vizuri, najivunia matokeo haya na kuwa sehemu ya historia ya soka la Tanzania," alisema Morocco.
Aliongeza pia anawashukuru sana wachezaji wake kwa kupambana na kufanikiwa kufuzu fainali hizo.
Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta, alisema anamshukuru Rais Samia kwa zawadi aliyowapatia na anamshukuru kwa nguvu kubwa anayotumia katika kuendeleza michezo nchini.
Samatta aliongeza wanashukuru mchango wa rais huyo kwa mchango ambayo ameutoa kwa Stars kuanzia huko nyuma hadi walipofanikiwa kufuzu fainali hizo kwa mara ya nne.
"Kwa niaba ya wachezaji, zawadi ambayo imetoka kwa mama, tunafahamu ni kipindi kipindi ambacho nchi inapitia, na yeye kama mama yetu, ni kipindi kigumu anapitia, tunamshukuru kwa zawadi hii, tunamshukuru kwa yote aliyoyafanya, tunamshukuru sana mama, tunajua unatuangalia, tunakuongeza kwa Mungu, aendelee kukupa afya na kuendelea kutujali na wengine wote unaowajali hapa Tanzania," Samatta alisema.
Jamhuri Julio, ambaye pia yuko katika benchi la ufundi la Stars, alisema umefika wakati makocha wazawa wakaaminiwa kwa sababu wana uwezo na uzoefu wa kuzipa mafanikio timu zetu.
Julio alisema anaamini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na wadau wengine wakiwaamini makocha kutoka hapa nchini, mafanikio yatapatikana na nchi inafika mbali.
"Umefika wakati makocha wazawa tukaaminiwa, uwezo na uzoefu tunao, ninawapongeza sana Morocco na Mgunda (Juma), kwa mafanikio haya, tuwape nafasi, hakuna ambacho makocha wakigeni wanacho na sisi makocha wazawa hatuna," Julio aliongeza.
Taifa Stars inaungana na Uganda (Uganda Cranes) na Sudan ambazo zimetoka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kufuzu kushiriki fainali hizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED