KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesifu kiwango kilichooneshwa na beki mpya wa kushoto wa Yanga, Israel Mwenda, kwenye mchezo wa Kombe la FA, uliopigwa, Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam dhidi ya Copco FC, akisema ujio wake na kile alichoonesha, kitaongeza nguvu kwenye timu kufikia malengo waliyojiwekea.
Ramovic alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, siku mbili baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Copco FC.
Katika mchezo huo, Mwenda, alicheza mechi yake ya kwanza tangu asajiliwe kutoka Singida Black Stars, huku akitoa pasi za mwisho mbili, akichangia ushindi wa idadi hiyo ya mabao dhidi ya timu hiyo yenye maskani yake jijini Mwanza.
"Huwa napenda kuzungumza habari ya timu kwa ujumla kila mara, kwa sababu wote sisi ni wamoja, tunafanya kazi pamoja, hatushindi mechi kwa mchezaji mmoja mmoja, bali timu.
"Kwa maana hiyo siwezi kusema mchezaji fulani amecheza vizuri zaidi na mwingine hajacheza vema, siwezi kuwatoa kasoro wachezaji wangu kwani tukishinda tunashinda pamoja na tukifungwa tunapoteza wote," alisema Ramovic na kuongeza:
"Nikirudi kumzungumzia Mwenda, ni kwamba anaonekana yupo vizuri, amefanya vema kwenye mchezo wetu, na hiki kwake ni kitu muhimu ili kutupa imani, anaonekana atatuongezea kitu kuelekea kwenye malengo yetu."
Akizungumza baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza akiwa na Yanga, Mwenda, alifurahi kuwa na mwanzo mzuri kwani si wachezaji wote wanaokwenda timu mpya na kufanya vizuri.
"Niwapongeze wachezaji wenzangu, ushirikiano ulikuwa muhimu katika mchezo wa kwanza, unajua ndiyo kwanza nimefika, lakini mwanzo nilioanza nao ni mzuri sana.
"Nilikuwa na hamu sana ya kupata nafasi, na nilipoipata nikasema leo ngoja niitumie ili watu wajue kuwa kuna mchezaji mpya amejiunga, unaposajiliwa kipindi cha dirisha dogo, hutakiwi kupewa muda, unaingia moja kwa moja kuisaidia timu," alisema Mwenda ambaye kabla ya kuwa Singida Black Stars, aliichezea Simba.
Mchezaji huyo alitoa 'asisti' mbili kwenye bao la Prince Dube, dakika ya 66, likiwa bao la pili kwenye mchezo huo na la tano dakika ya 84, lililounganishwa kwa kichwa na Mudathir Yahaya.
"Katika 'asisti' hizo nimependa ile ya pili, maana Kibwana Shomari aliniwekea kwenye njia kwa wakati sahihi na mimi nilikuwa kwenye mwendo, nilichofanya nikapiga krosi iliyokuwa na malengo mawili, ikimkuta mtu afunge au wao wajifunge wenyewe kwenye harakati za kuokoa," alisema Mwenda.
Yanga iliongeza wachezaji wawili tu kipindi cha dirisha dogo la usajili, ambapo mbali na Mwenda, yumo pia, Jonathan Ikangalombo, winga aliyesajiliwa kutoka AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambaye hakucheza mechi hiyo, na kwa mujibu wa kocha Ramovic, alikuwa mgonjwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED