Pamba yapigwa faini mil. 5/- kisa Simba, Minziro atamba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:50 AM Dec 03 2024
Pamba yapigwa faini mil. 5/-   kisa Simba
Picha:Mtandao
Pamba yapigwa faini mil. 5/- kisa Simba

BAADA ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KenGold juzi, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fred Felix Minziro, amesema sasa gari limewaka, huku klabu hiyo ikitozwa faini ya Sh. milioni tano kwa kosa la baadhi ya maofisa wake kuingilia mazoezi ya timu ya Simba.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, alisema ushindi huo, ukijumlisha na uliopita walivyoifunga Fountain Gate mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara, na kufungwa kwa tabu bao 1-0 dhidi ya Simba Novemba 22 , mwaka huu, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, inaonesha kuwa kikosi chake kimeimarika kwa kiasi kikubwa tofauti na kilivyoanza ligi.

"Nadhani sasa tumeimarika si kama tulivyoanza ligi, nimeendelea kukiimarisha siku hadi siku, matokeo ya hivi karibuni yanaonesha hilo, tumebakisha michezo miwili tumalize mzunguko wa kwanza, nadhani huko mbele hatutokuwa hivi tena, tutaendelea kuimarika zaidi," alisema kocha huyo.

Akiuzungumzia mchezo huo alisema haukuwa rahisi, lakini anawashukuru vijana wake kwa kupambana na kupata ushindi huo uliowasogeza juu kidogo ya msimamo.

"Mechi haikuwa rahisi, presha ilikuwa juu, nawashukuru vijana wangu kwa kupambana hadi tumepata ushindi ambao utawafanya warudishe morali na kujiamini zaidi katika michezo ijayo," alisema.

Kocha Mkuu wa KenGold, Omari Kapilima, alisema matokeo hayo hakuyatarajia, kwani alijipanga kushinda au kupata sare ugenini.

"Matokeo sikuyatarajia, lakini ni moja ya matokeo ya mchezo wa soka. Nilipanga mipango ambayo haikukubali, nikabadilisha wachezaji watatu kipindi cha kwanza, hata hivyo haikusaidia tukapoteza kwa bao 1-0, bado nina kazi ya kufanya kwenye mazoezi kurekebisha hali hii," alisema.

Matokeo hayo yanaifanya Pamba Jiji kupanda hadi nafasi ya 12 ya msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 11 kwa michezo 13 iliyocheza, huku KenGold, ikiburuza mkia ikiwa na pointi sita kwa michezo 13 iliyocheza mpaka sasa. Timu zote hizo zimebakisha michezo miwili kila moja ili kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.

Wakati huo, klabu hiyo imetozwa faini kiasi cha Sh. milioni tano, baada ya baadhi ya maofisa wake kuingilia mazoezi ya timu ya Simba siku moja kabla ya mchezo baina yao uliochezwa, Uwanja wa CCM Kirumba, Novemba 22, mwaka huu Wekundu wa Msimbazi walipondoka na ushindi wa bao 1-0.

Taarifa iliyotolewa jana na Bodi ya Ligi, imesema maofisa wa timu hiyo walionekana uwanjani katika muda wa kikanuni wa timu hiyo kufanya mazoezi.

Bodi imesema maamuzi hayo yamefanywa na Kamati ya Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB).