Mwana FA: Tukutane Betika Mbeya Tulia Marathon 2024

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:12 AM May 07 2024
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA, akiwakabidhi bendera ya mabingwa baadhi ya wanariadha wa Dar es Salaam jana, watakaokimbia mbio za Betika Mbeya Tulia Marathon Ijumaa na Jumamosi wiki hii jijini Mbeya.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA, akiwakabidhi bendera ya mabingwa baadhi ya wanariadha wa Dar es Salaam jana, watakaokimbia mbio za Betika Mbeya Tulia Marathon Ijumaa na Jumamosi wiki hii jijini Mbeya.

NAIBU Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA, amefichua namna alivyojipanga kukimbia kwenye mbio ya Betika Mbeya Tulia Marathon msimu huu, akiwataka wadau wa riadha nchini wakutane Mbeya zinapofanyika mbio hizo.

Mwana FA amesema yuko fiti kukimbia na kumaliza mbio ndefu kwenye msimu wa saba wa Betika Mbeya Tulia Marathon Ijumaa na Jumamosi hii pale kwenye Uwanja wa Sokoine.

Akizungumza katika mbio za amshaamsha ambazo ni maalum kwa ajili ya maandalizi kuelekea Mbeya, Mwana FA aliyewaongoza mamia ya wanariadha wa jijini Dar es Salaam kwenye amshaamsha hiyo alisema, morali ambayo wanariadha hao wameionyesha hakuna shaka Mbeya ushindani utakuwa mkali.

Mbio za Betika Mbeya Tulia Marathon zinazolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya na elimu zitaongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Zaidi ya wakimbiaji 5000 watakimbia kusaka mabingwa wa marathon (kilomita 42), nusu marathon (kilomita 21) kilomita 10 na kilomita tano Jumamosi wiki hii, ikiwa ni siku moja baada ya mbio za uwanjani za mita 100, 200, 400, 800 na 1500.

Japo hakusema atakimbia mbio gani, Naibu Waziri huyo alisema atakimbia mbio ndefu na hana shaka atafanya vizuri, kauli kama iliyowahi kutolewa na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson katika amshaamsha kama hiyo iliyofanyika jijini Dodoma hivi karibuni, akibainisha yuko fiti kwa marathon na atashinda medali.

Katika amsha amsha hiyo iliyoanzia kwenye ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere, Posta hadi kwenye fukwe za Coco, Mwana FA alibainisha alivyofiti kukimbia na kumaliza mbio ndefu bila kueleza ni za kilomita 10, 21 au 42.

"Tukutane Mbeya, niko fiti, kama Dar es Salaam nimekimbia na kumaliza umbali mrefu, kule Mbeya mjipange," alisema Naibu Waziri huyo akishangiliwa kwa nguvu huku baadhi ya wanariadha wa Dar es Salaam wakiahidi kurudi na ubingwa.

Baadhi ya wanariadha wa Dar es Salaam wamepata udhamini wa Betika kwenda kuchuana jijini Mbeya wakilipiwa usafiri na gharama nyingine, ikiwa ni sehemu ya kampuni hiyo ya michezo ya kubashiri matokeo ambao ndio wadhamini wakuu wa kuzinogesha mbio hizo msimu huu.

Ofisa Habari wa Betika, Rugambwa Juvenalius, alisema amshaamsha hiyo kesho Jumatano itafanyika jijini Mbeya, ikiwa ni baada ya mikoa ya Mtwara, Rukwa, Iringa, Morogoro na Dodoma kufanya tukio kama hilo kama sehemu ya maandalizi ya kushiriki mbio za msimu huu.

Alisema, Betika itawagharamia wanariadha 460 kushiriki mbio hizo msimu huu, kuongeza hamasa na kutoa fursa kwa wale wenye vipaji kuonekana.