Mabao 39 yafungwa Ligi Kuu, matano nje ya boksi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:40 AM Sep 19 2024
Mpira golini.
Picha: Mtandao
Mpira golini.

KATIKA hali inayoonyesha bado kuna udhaifu wa wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara kupiga mashuti ya mbali, jumla ya mabao 39 yaliyofungwa msimu huu na nyota 30, ni matano yamefungwa nje ya eneo la hatari.

Kwa mujibu wa dawati la takwimu la Nipashe, mabao 34 yamefungwa ndani ya kiboksi cha hatari.

Wakati mabao matano yakifungwa nje ya boksi, mabao saba yamefungwa kwa kichwa, huku straika wa Singida Black Stars, Elvis Rupia, akiaongoza kwa kufunga magoli mawili kwa njia hiyo.

Waliofunga mabao nje ya boksi mpaka sasa ni Emmanuel Keyekeh wa Singida Black Stars, Velentino Mashaka (Simba), Maxi Nzengeli (Yanga), Redemtus Mussa (KMC) na Dickson Ambundo wa Fountain Gate.

Mbali na straika raia wa Kenya, Rupia kuongozwa kwa kufunga mabao mawili ya vichwa, wengine ni Mohamed Damaro wa Singida Black Stars, Che Fondoh Malone, Mashaka na Edwin Balua kutoka Simba, na Redemtus wa KMC.

Jumla ya penalti sita zimeshatolewa mpaka sasa, nne zikitinga nyavuni na mbili zikiota mbawa.

Takwimu za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaonyesha katika michezo 25 iliyochezwa mpaka sasa, mechi 16 zimetoa mshindi na tisa timu zimetoka sare.

Hali inaonyesha timu zimejipanga msimu huu kupata ushindi popote pale, mechi nane zimetoa ushindi nyumbani na idadi hiyo hiyo imetoa washindi waliokuwa ugenini.

Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mchezo mmoja kati ya Azam FC, itakayokwenda kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kucheza dhidi ya wenyeji KMC.

Wakati Azam FC ikiwa na pointi mbili tu baada ya kutoa suluhu dhidi ya JKT Tanzania na Pamba Jiji ikiwa nafasi ya 12, KMC ipo nafasi ya saba ikikusanya pointi nne.