Biashara ya China-Tanzania yafikia dola bilioni 8.7 kwa miaka 23

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 10:10 PM Sep 19 2024
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjianakizungumza na waandishi wa habari katika khafla iliyoandaliwa kutoa mrejesho wa kikao cha FOCAC
Picha: Mwandishi wetu
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjianakizungumza na waandishi wa habari katika khafla iliyoandaliwa kutoa mrejesho wa kikao cha FOCAC

BALOZI wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema biashara kati ya China na Tanzania imeongezeka kutoka chini ya dola milioni 100 hadi dola bilioni 8.78 kuanzia mwaka 2000 hadi 2023 kutoka na ushirikiano uliopo.

Balozi Mingjian aliyasema hayo  jijini Dar es Salaam alipokuwa  akizungumza na waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhusu matokeo ya Mkutano wa FOCAC uliofanyika China hivi karibuni.

Balozi alisema ushirikiano kati ya China na Tanzania umekuwa ukiongoza kwa muda mrefu na wamepata matokeo mazuri kutokana na uwekezaji wake nchini Tanzania na kunufaika na FOCAC.

"Kama mwanachama muhimu wa FOCAC, Tanzania imehudhuria kwa shauku katika shughuli za forumu hiyo na kusaidia maendeleo yake. Tangu kuanzishwa, biashara kati ya China na Tanzania imeongezeka kutoka chini ya dola milioni 100 hadi dola bilioni 8.78 kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2023, ongezeko la karibu mara 88," alisema.

Aidha, alisema ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini China ilikuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa alikutana na Rais wa China, Xi Jinping, ambaye alibainisha kuwa nchi yake iko tayari kuifanya Tanzania kuwa eneo la onyesho la kuimarisha ushirikiano wa hali ya juu wa China-Afrika chini ya Mpango wa Ukanda na Barabara (BRI).

Alisema china iliahidi kuendelea kusaidia nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ujenzi wa miradi mbalimbali ya elimu, afya na miundombinu kwa Tanzania na Zambia zitasaidiwa kuendeleza reli ya Tazara ambayo China ndiyo ilikuwa mwasisi wake kwa kujitolea.

Balozi Mingjian alisema  reli hiyo imekuwa kiunganishi kikubwa cha China na Tanzania,  hivyo tunapotaja uhusiano wa nchi hizo huwezi kuacha kuitaja hivyo wataiendeleza kama ambavyo kupitia mkutano huo Zambia, Tanzania zilikuwa na kikao .maalumu cha kujadili uendelezaji wa miradi huo muhimu kiuchumi.

Aidha, alisema ni muhimu kuzingatia kuwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) hivi karibuni kilifanya kikao chake cha tatu cha kamati kuu ya 20 kilipitisha azimio la kusonga mbele na mageuzi zaidi. Uamuzi huu unaweza kuwa na matokeo makubwa.

Naye Mhadhiri Mwandamizi  wa Chuo cha Mipango,  Dk.Bonamax Mbasa, alisema mkutano wa FOCAC umekuwa na tija kubwa kwa viongozi wa nchi za Afrika, kutokana na mipango mizuri na mikakati iliyowekwa, hivyo wanatakiwa kujitatsmini  na kujipanga kufikiria namna ya kuyatekeleza.