Fadlu na hesabu kali za kuiliza Tabora Utd

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:25 AM Jan 28 2025
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema alikuwa uwanjani kuiongoza timu yake ikicheza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Kilimanjaro Wonders, lakini akili yote ikiwaza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tabora United, utakaopigwa Jumapili wiki hii katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.

Akizungumza juzi baada ya timu yake kuibugiza Kilimanjaro Wonders mabao 6-0 na kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ya michuano ya FA, Fadlu, alisema aliutumia mchezo huo ili kuwapa nafasi wachezaji wake wote ambao hawapati muda wa kucheza kwenye Ligi Kuu, kupata dakika za kucheza, wakati huo huo akiweka sawa silaha zake anazozitegemea kwenye mchezo unaofuata.

"Ilikuwa ni mechi muhimu kwa wachezaji wote kupata muda wa kucheza, hasa ambao hawakuwa wanapata nafasi, ni kweli kuna baadhi ya wachezaji hawakuwapo, Aishi Manula amepatwa na mafua, wengine walikuwapo, lakini ilibidi niwapumzishe kwa sababu tuna mchezo mgumu dhidi ya Tabora United," alisema Fadlu.

Alisema hata mchezo huo ulikuwa ni kama sehemu tu ya maandalizi ili kuangalia baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa hawaanzi mara kwa mara kuwatumia kuongeza nguvu kwenye mechi hiyo pindi itakapohitajika.

"Tumeutumia kama mazoezi, tunaangalia wachezaji ambao wamekuwa na viwango vya kutosha kuweza kuongeza nguvu katika mchezo wetu huo muhimu wa Ligi Kuu, pale wanapohitajika kuingia uwanjani kwenda kufanya kile ambacho tumewatuma," alisema Fadlu, raia wa Afrika Kusini.

Akiuzungumzia mchezo huo, alisema wamecheza na timu ambayo kiwango chao ni tofauti kabisa na cha Simba, ila baadhi yao wana vipaji.

"Vijana hawa wa Kilimanjaro Wonders ni wachanga, walijitahidi kwa kadri ya uwezo wao, lakini viwango vya timu na vya mchezaji mmoja mmoja vilikuwa tofauti kabisa, ila nimeona baadhi wana vipaji," alisema.

Kocha Msaidizi wa timu ya Kilimanjaro Wonders, Wilbard Pacho, alisema lengo lao kubwa lilikuwa ni kupata angalau bao moja la kufutia machozi, lakini kwa bahati mbaya walilikosa.

"Tuliangalia ubora na udhaifu wa Simba, lakini tulikuja hapa angalau tupate bao moja au mawili, watufunge lakini mabao 3-1, 5-2, hatukutaka tutoke uwanjani bila bao la kufutia machozi, lakini ubora wa wachezaji wa Simba umetuadhibu," alisema.

Hata hivyo, alisema wamepata nafasi ya kujifunza, na hilo litawasaidia kwenye mechi zao watakazocheza.

"Wachezaji wetu ni vijana wadogo hawana ukomavu, kwa mechi hii tumejifunza, na hili ndilo tulikuwa tunahitaji, kama wameweza kupambana na Simba na kupelekeshwa kwa kasi ile, nadhani watakuwa wamekomaa na kujifunza kwani hakuna timu yoyote ya levo yetu inayoweza kucheza kama hivi, ila na sisi tutakwenda kuzipelekesha kama Simba ilivyotufanyia," alisema.

Mabao ya Simba yalifungwa na Velentino Mashaka, Ladack Chasambi, Joshua Mutale, Steven Mukwala, Edwin Balua na moja la kujifunga wenyewe kupitia kwa Patrick Sebastian.