KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davis, amesema ifikapo Februari mwakani, kikosi chake kitakuwa moto wa kuotea mbali si Tanzania tu bali hata kwenye michezo ya kimataifa barani Afrika, akiwataka wote wanaotoa maoni yao juu ya kikosi hicho kusubiri mpaka wakati huo.
Akizungumza jijini Dar es Saaam jana, raia huyo wa Afrika Kusini, alisema licha ya kwamba tayari atakuwa ameshaongeza wachezaji kipindi cha usajili wa dirisha dogo, lakini kitaalamu, atakuwa ameshakinoa kikosi hicho kwa muda wa miezi sita huku kikiwa kinapambana uwanjani.
"Kitaalamu ni kwamba klabu yoyote inaposajili kiasi cha wachezaji 15 na kocha mpya inatakiwa miezi sita ili kuona kiwango halisi cha timu na muunganiko wa wachezaji, kwani watakuwa wameshaelewana mikimbio, mifumo, sifa na udhaifu wa kila mchezaji ili kusaidiana uwanjani, tulianza ligi na michuano ya kimataifa Agosti, tukiwa na kikosi kichanga kinachojengwa, kipindi hiki tunamalizia ujenzi, lakini mabadiliko yanaonekana," alisema kocha huyo.
Alisema kwa michezo minane ya Ligi Kuu ambayo timu yake imecheza mpaka sasa, na miwili ya Kombe la Shirikisho, inaonekana inapiga hatua, lakini bado mpaka Februari mwakani ndipo kikosi hicho kitakuwa kimeshakamilika vile inavyotakiwa kitaalamu.
"Kuna mabadiliko makubwa sana kwenye kikosi changu, unaweza kuona sasa baadhi ya wachezaji wameanza kuelewana na wenzao, wanaweza kupiga pasi ambazo wanajua wenzao wanaweza kuzifikia, kila mchezaji ana aina yake ya kupigiwa pasi, mikimbio, kutafuta nafasi, hilo wachezaji wangu wengi walikuwa hawajajuana, lakini kila wanapocheza kuna kitu kipya wanakuja nacho.
Unaweza kuona sasa kila mtu ana spidi, hata wale ambao wamekuwa hawapati nafasi sasa wako fiti na utimamu wa mwili ambapo mwanzo walikuwa wanavikosa, mfululizo wa michezo umesababisha nibadilishe baadhi ya wachezaji ambapo imekuwa na faida sana kwetu, tayari nimeona tuna kikosi kipana cha wachezaji wanaoweza kucheza uwanja kama wale ambao wapo nje, hili limeonekana katika mchezo wetu uliopita dhidi ya Namungo," alisema kocha huyo.
Fadlu alibainisha mpaka ikifika muda ambao unatakiwa, Simba itakuwa moto wa kuotea mbali na kuwa tayari kucheza na timu yoyote ile Afrika, akiwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kufurahi yale maneno kuwa timu bado inajengwa hayatokuwapo tena.
Simba ambayo ina idadi kubwa ya wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu baada ya kuondoa rundo la wachezaji wengi wakongwe, imecheza michezo rasmi 10, minane ya Ligi Kuu na miwili ya kimataifa.
Katika michezo hiyo, imeshinda saba, sare mbili na kupoteza mmoja tu dhidi ya Yanga kwa bao 1-0, ambao ulipigwa Oktoba 19, mwaka huu.
Wakati inacheza michezo hiyo, Fadlu, amekuwa akisisitiza kuwa kikosi chake bado hakijawa sawa kimuunganiko, lakini akiwashangaza wengi kwani pamoja na upya na kukosa muunganiko kimekuwa na mabadiliko tofauti na cha misimu miwili iliyopita, ambapo mbali na kukonga nyoyo ya wanachama na mashabiki kutokana na kinavyocheza, lakini kimekuwa kikipata ushindi kwenye michezo mingi kinayocheza.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED