Dube: Nataka kushinda makombe

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:14 AM Jul 10 2024
Prince Dube(katikati).
Picha: Yanga
Prince Dube(katikati).

MSHAMBULIAJI mpya wa klabu ya Yanga, Prince Dube, amesema anaamini anaweza kushinda mataji akiwa na mabingwa hao watetezi.

Nyota huyo jana aliungana na wachezaji wengine kuanza maandalizi yao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.

Akizungumza na gazeti hili, Dube aliyejiunga na Yanga akitokea Azam FC, alisema lengo lake ni kuona anashinda taji la Ligi Kuu msimu ujao na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.

"Nipo tayari kutoa mchango wangu kwenye timu, naamini naweza kutwaa mataji nikiwa na Yanga... tumeanza maandalizi na nitahakikisha najituma kwa ajili ya timu," alisema nyota huyo raia wa Zimbabwe.

Alisema Yanga ina wachezaji wazuri na wenye uzoefu hivyo ana uhakika kama watajituma wanaweza wakatetea tena ubingwa wao wa Ligi Kuu.

Kabla ya kujiunga na Yanga, Dube alikuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Azam kabla ya kuomba kuondoka ndani ya timu hiyo na kujiunga na Yanga.

Dube pia alikuwa akiwindwa na klabu ya Simba kabla ya kuamua kumwaga wino kuwatumikia mabingwa hao wa nchi.