KLABU ya Coastal Union imekana kutaka kumrudisha kocha wake wa zamani, Juma Mgunda ili kukinoa kikosi hicho.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Abbas El Sabri, amesema taarifa za Mgunda kutaka kurejea Coastal Union si za kweli, lakini akakiri kuwa viongozi wapo kwenye mchakato wa kusaka Kocha Mkuu na watu wa benchi la ufundi.
Sabri, alisema Coastal imelazimika kutoa ufafanuzi huo kutokana na taarifa nyingi ambazo zinaihusisha timu hiyo na Mgunda, ambaye amemaliza mkataba wake wa miaka miwili na klabu ya Simba.
"Hakuna taarifa yoyote juu ya Juma Mgunda kwenye klabu yetu, tunajua yeye alikuwa mchezaji wetu zamani na alihudumu kwa mafanikio makubwa, pia alikuwa kocha na kufanya mambo makubwa, kusema hatumuhitaji ni kumkosea heshima, lakini kwa sasa hakuna mipango hiyo ya kuzungumza naye, badala yake uongozi bado unaendelea na mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu na watu wa benchi la ufundi, lakini siyo Mgunda, timu iko chini ya Kocha Joseph Lazaro ambaye anakaimu na amekuwa akifanya vizuri na viongozi wameonyesha kuwa na imani naye," alisema El Sabri.
Tetesi zinasema kuwa klabu zilizokuwa zikimtolea macho Mgunda ni Coastal na Namungo.
Kabla ya kutua Simba, Mgunda alikuwa kocha wa Coastal na alichukuliwa kuziba nafasi ya Zoran Maki ambaye aliondoka mapema kwenye klabu hiyo kabla ligi wala michezo ya kimataifa haijaanza, aliiwezesha kutinga hatua ya makundi, Ligi ya Mabingwa Afrika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED