UONGOZI wa Copco FC inayojiandaa kuivaa Yanga katika mechi ya raundi ya tatu ya mashindano ya Kombe la FA itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam imesema wachezaji wake watatumia mchezo huo kusaka nafasi ya kusajiliwa na vigogo hao.
Kauli hiyo pia imeungwa mkono na mabosi wa Kilimanjaro Wonders ambayo itacheza Jumapili itawakabili Simba katika mashindano hayo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa timu hizo wameonekana kufurahia kucheza na vigogo hao licha ya ugumu ambao wanatarajia kukutana nao katika mechi hizo.
Meneja wa Copco, yenye maskani yake jijini Mwanza, Juma Kisuse, alisema kikosi cha wachezaji 20 na viongozi saba wa timu hiyo kiko kamili Dar es Salaam tayari kwa mchezo huo, huku akisema ni fursa adhimu kucheza na Yanga.
"Yanga ni timu kubwa, ambayo kila mtu anatamani kucheza nayo, tumepata nafasi ya kucheza nayo, hii ni fursa nzuri ya wachezaji wangu kufanya vitu vizuri, kuonyesha uwezo katika mchezo huo ili kupata nafasi ya kujiuza, nimewaambia wapambane ili wapate soko, kama si kwa timu hiyo basi nyingine ambazo zitakuwa zinaangalia mechi hiyo," Kisuse alisema.
Aliongeza ili kujiimarisha kuwakabili mabingwa hao watetezi, kikosi chake kimecheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Pamba Jiji.
"Maandalizi yetu ni mazuri na ndiyo maana tukaamua kujipima na Pamba Jiji kwa sababu timu hiyo na Yanga zote zipo Ligi Kuu," alisema Kisuse, meneja wa timu hiyo inayoshiriki First League zamani Ligi Daraja la Pili.
Naye Mkurugenzi wa Kilimanjaro Wonders, Laurent Kinabo, alisema kwao kucheza dhidi ya Simba ni fursa kubwa ambayo itawafanya wachezaji wake baada ya hapo kujiamini kucheza na timu yoyote ile.
"Hii ni fursa kubwa sana kwetu kucheza na Simba, mechi hii itawatengenezea wachezaji wangu kuanza kujiamini, pia matumaini ya kutimiza ndoto zao kupitia mechi hiyo, wanahitaji kujituma na kuonyesha walichonacho ili kupata soko la usajili msimu ujao," alisema Kinabo, ambaye timu yao inashiriki Ligi ya Mkoa Kilimanjaro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED