Wanamichezo bora wa kuangaliwa mwaka 2025

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:30 AM Dec 30 2024
Mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe
Picha: Mtandao
Mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe

KALENDA ya michezo inapozidi kupamba moto kuelekea mwaka 2025, ulimwengu unatazamiwa kuona msururu wa matukio ya kusisimua na burudani za kila aina.

Kuanzia mashindano ya Riadha ya Dunia, Ndondi na Ligi Kuu ya England, kuna burudani kwa kila mtu.

Hii ni orodha ya wanamichezo wa kuangaliwa mwaka 2025, kuanzia kwenye mpira wa miguu, kikapu, riadha hadi ndondi, twende sasa...

Lamine Yamal

Mchezaji wa Barcelona na Hispania, Lamine Yamal ameshinda tuzo ya Golden Boy mwaka 2024.

Tuzo hiyo iliyoanzishwa na gazeti la Italia la Tuttosport, hutolewa kwa mchezaji bora wa Ulaya kwa wanaume chini ya umri wa miaka 21, huku waandishi wa habari wakipiga kura kwa kutumia mfumo wa pointi.

Yamal mwenye umri wa miaka 17, alijiimarisha katika kikosi cha kwanza cha Barcelona msimu uliopita kabla ya kuisaidia Hispania kushinda Euro 2024.

Winga huyo alifunga bao moja na kusaidia mengine manne huku akitajwa kuwa mchezaji chipukizi bora wa michuano hiyo.

Mnamo Oktoba, Yamal alishinda tuzo ya Kopa, zawadi sawa na iliyotolewa wakati wa sherehe ya Ballon d'Or ya 2024.

Yamal amefunga mabao sita na kutoa asisti nane katika mechi 16 za mashindano yote msimu huu.

Faith Kipyegon

Bingwa wa Dunia wa Michezo ya Olimpiki kwenye Riadha, Faith Kipyegon, alikuwa na msimu mzuri mwaka 2023 aliposhinda mbio zake na kuweka rekodi tatu za dunia.

Kipyegon alivunja rekodi za dunia katika mbio za mita 1,500, 5,000 na kushinda mara mbili medali ya dhahabu ya mbio za mita 1,500 na 5,000 kwenye mashindano ya Dunia.

Pia alipata tuzo ya Mwanariadha Bora wa Kike wa 2023.

Kuelekea 2025, Kipyegon anapendelea zaidi kushinda medali za dhahabu katika mbio za mita 1,500 na kuna matumaini kwamba rekodi zaidi atazifikia.

Noah Lyles

Noah Lyles ni mwanariadha wa Marekani ambaye alijulikana kama "mtu mwenye kasi zaidi duniani" baada ya kushinda medali tatu za dhahabu katika mita 100, mita 200, na Relay ya mita 4 × 100 kwenye mashindano ya dunia ya mwaka 2023.

Lyles pia alishinda mbio za mita 100 kwa wanaume kwenye Michezo ya Olimpiki ya 2024, akimshinda Kishane Thompson wa Jamaica.

Kylian Mbappe

Kiwango cha mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe "kiko chini kwa sasa" lakini ana dhamira ya kuvuka kipindi kigumu, kwa mujibu wa kocha wake, Carlo Ancelotti.

Fowadi huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 25, ambaye alijiunga na Real kwa uhamisho wa bila malipo kutoka Paris St-Germain Julai, mwaka huu, amekuwa na wakati mgumu tangu alipowasili pale kwenye dimba la Bernabeu.

"Mbappe yuko chini kama kila mtu mwingine, lakini ana ari ya kumaliza kipindi hiki," alisema bosi wa Real, Ancelotti akiwaambia waandishi wa habari.

"Tatizo alilonalo ni la kila mtu. Unaweza kumwelekeza Vinicius Junior], Rodrygo au Jude Bellingham. Ni wakati mgumu kwa kila mtu."

Mchezaji huyo anatarajiwa kuimarika zaidi mwaka 2025 wakati ambapo atakuwa amefahamiana vizuri kimchezo na wachezaji wenzake wa Real Madrid.

Beatrice Chebet

Beatrice Chebet ni mwanariadha wa Kenya wa mbio ndefu ambaye ndiye anayeshikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 10,000 na medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya 2024 katika mbio za mita 5000 na 10,000, mbali na kuwa mwanamke wa tatu katika historia kushinda mbio mbili tofauti kwenye michezo ya Olimpiki.

Mwaka 2022, Chebet alishinda medali za dhahabu katika mbio za mita 5000 kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola, mashindano ya Afrika, na Ligi ya Diamond na medali ya fedha katika mbio za mita 5000 kwenye mashindano ya Dunia. Chebet pia alishinda medali za dhahabu katika mashindano ya Dunia ya 2023 na 2024.

Katika mashindano ya vijana, Chebet alishinda medali za dhahabu katika mbio za mita 5000 kwenye mashindano ya Dunia chini ya umri wa miaka 20 ya IAAF 2018 na sehemu ya Wanawake ya Vijana ya Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika za 2019.

Gervonta Davis

Gervonta Bryant Davis anayejulikana pia kwa jina lake la utani 'Tank', ni bondia wa Marekani. Ameshikilia taji la WBA uzito mwepesi tangu 2023. Pia alishikilia taji la Shirikisho la Ndondi la Kimataifa (IBF) mwaka 2017, taji la WBA super featherweight mara mbili kati ya 2018 na 2020, na taji la WBA la uzito mwepesi mwaka 2021.

Kufikia Mei 2024, Davis aliorodheshwa kama mchezaji wa pili bora zaidi duniani katika uzani mwepesi na ESPN.

Bondia huyo ana mpango wa kustaafu mwaka 2025, na kuacha historia ambayo imewashangaza mashabiki wengi.

Victor Wembanyama

Nyota wa timu ya mpira wa kikapu ya Marekani, San Antonio Spurs, Victor Wembanyama ameshinda tuzo ya mchezaji bora anayechipukia wa NBA mwaka huu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20, ndiye Mfaransa wa kwanza kushinda tuzo hiyo baada ya kuwa na wastani wa pointi 21.4

Wembanyama, alipata kura zote 99 za nafasi ya kwanza.

Letsile Tebogo

Letsile Tebogo ni mwanariadha kutoka Botswana. Alishinda medali ya dhahabu katika Olimpiki ya 2024 kwenye mashindano ya mbio za mita 200, na ushindi wake uliipatia Botswana dhahabu ya kwanza ya Olimpiki. 

Pia alishinda medali ya fedha katika mashindano ya Dunia ya 2023 katika mbio za mita 100 na kufuatiwa na medali ya shaba katika mbio za mita 200 siku tano baadaye.

Tebogo alishinda katika mbio za mita 100 na kushika nafasi ya pili kwenye mbio za mita 200 katika mashindano yote mawili ya Riadha ya Dunia ya 2021 na 2022. Mwaka 2021, alikua mwanariadha wa kwanza wa Botswana kushinda taji la mita 100 katika kiwango chochote cha ubingwa wa Dunia. 

Yeye ndiye bingwa wa Afrika wa mita 200 mwaka 2022 na kuwa mshindi mwenye umri mdogo zaidi wa taji hili katika historia ya mashindano. Alishinda tuzo ya mwanamichezo bora wa dunia upande wa wanaume 2024.

Amos Serem

Mwanariadha Mkenya Amos Serem alisitisha mfululizo wa ushindi wa miaka miwili wa ubingwa wa Olimpiki, Soufiane El Bakkali na kushinda taji lake la kwanza la Ligi ya Diamond la mbio za mita 3000 kuruka viunzi kwenye fainali ya Allianz Memorial van Damme – Wanda Diamond League mjini Brussels nchini Ubelgiji.

Serem alimzidi El Bakkali kwa urahisi katika awamu ya mwisho na kushinda kwa saa 8:06.90. El bakali wa Morocco alimaliza katika nafasi ya pili kwa muda wa 8:08.60 huku Mohamed Amin Jhinaoui wa Tunisia (8:09.68) akimaliza wa tatu.

Daniel Dubois

Daniel Dubois ni mwanamasumbwi mtaalam wa England. Ameshikilia taji la uzani mzito la Shirikisho la Ndondi za Kimataifa (IBF) tangu Juni 2024. Hapo awali, aliwahi kushikilia taji la uzito wa juu la Chama cha Ngumi cha Dunia (WBA) kutoka 2022 hadi 2023.

Akiwa mwanariadha, alikuwa bingwa mara tano wa England kwa upande wa vijana. Dubois anajulikana kwa uwezo wake wa ngumi nzito akishinda mara 21 kati ya 22 kwa njia ya knockout.

Ushindi wake mkubwa ni dhidi ya bingwa wa zamani wa uzani mzito zaidi duniani, Anthony Joshua.

Faith Cherotich

Faith Cherotich ni mwanariadha wa Kenya ambaye ni mtaalam wa mbio za mita 3000 za kuruka viunzi. Akiwa na umri wa miaka 17, alishinda tuzo ya shaba katika mashindano ya riadha ya Dunia ya walio chini ya umri wa miaka 20 ya 2021 yaliyoandaliwa Nairobi nchini Kenya.