VUGUVUGU la mageuzi ya kidemokrasia lililobadili mfumo wa siasa na kubatilisha itikadi za chama kimoja au chama dola, mwakani linashuhudia miaka 30 ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi.
Kazi ya kutaka kuwapo na mbadala wa CCM haikuwa nyepesi. Ikianza miaka ya 1980 vuguvugu hilo liliratibiwa na wanaharakati vijana, wanasiasa wakongwe na wazee pia wakiwamo James Mapalala, Chifu Abdallah Fundikira, Balozi Kasanga Tumbo, Kasela Bantu na Lifa Chipaka, Emmanuel Makaidi, Mashaka Chimoto na Mchungaji Christopher Mtikila.
Wanaharakati wa kidemokrasia hawa wanaokumbukwa kutaka Tanzania ya vyama vingi leo hawapo duniani.
Hata hivyo, jukumu hilo hawakulifanya peke yao, walikuwapo wanamageuzi wengine vijana kama Mabere Marando, Ndimara Tegambwage, Prince Bagenda na Ringo Tenga waliokuwa wakishiriki na kuunga mkono juhudi hizo.
Wanasheria machachari (wote marehemu) Dk. Masumbuko Lamwai na Dk. Sengondo Mvungi nao watakumbukwa kwa michango yao ya kusimamia na kutaka Tanzania yenye sauti za vyama vingi ikichomoza kuanzia wakati huo.
Mbali na hao, walikuwamo vijana wasomi wa wakati huo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama Ludovick Bazigiza, Haroun Kimaro, Omary Kimweri, Jasson Kaishozi waliofukuzwa chuo mwaka 1989 na wote wameshafariki dunia.
Wenzao waliokuwa nao katika kundi hilo na kufukuzwa chuo kikuu, ni James Mbatia, Mosena Nyambabe, Cleven Mmary, Fabian Rutalemwa na Rwekama Rweikiza. Hawa ni wana harakati za kisiasa ambao kazi zao zinaendelea kuakisi demokrasia.
MWANZO WA HARAKATI
Mwaka 1984, mmoja wa wana mageuzi hao James Mapalala, alijilipua kwa kuandika barua ya wazi kwa Rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Julius Nyerere, kutaka mabadiliko kwa kuachana na mfumo wa chama kimoja cha siasa wakati huo CCM na kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Ilikuwa ngumu kwa Nyerere kupokea wazo hilo, mwandishi wa barua hiyo aliishia kizuizini hadi mwaka 1989 alipoachiwa, lakini akaendelea na vuguguvu hilo la mageuzi ya kisiasa ambalo lilikuwa limesambaa duniani kote.
Kutokana na upepo huo wa mageuzi ulivyokuwa umeshika kasi, Mwalimu Nyerere alitamka kwamba si vibaya Tanzania nayo ikaanza kujadili suala la mfumo wa vyama vingi, mwaka 1991 wana mageuzi 10 walikutana Dar es Salaam, kujadiliana mikakati na kuweka mipango ya kuanza hatua hiyo, ukawa mwanzo wa kuzaliwa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ikipewa jina la National Committee for Constitutional Reform (NCCR).
Kamati hiyo iliongozwa na Chifu Abdallah Said Fundikira, huku katibu wake mkuu akiwa Mabere Marando wakati Zanzibar ikiitwa Kamati ya Uhuru wa Kisiasa (KAMAHURU).
Baadaye kilichofuata ni mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam kupewa taarifa ya kikao cha wanamageuzi hao, Mashaka Chimoto akipewa jukumu la kuwasomea waandishi maamizio ya mkutano.
Wakati akiyasoma na ujumbe ukiwa ni kutaka kuwapo vyama mbadala wa CCM, alikumbana na vyombo vya dola na kutiwa mikononi mwa polisi pamoja na wenzake akiwamo Prince Bagenda na Ndimara Tegambwage.
Baada ya kuzidi kwa harakati hizo za mageuzi, Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi (hayati), aliunda Tume ya Jaji Francis Nyalali, kupata maoni ya Watanzania kama wako tayari kuanzishwa siasa za vyama vingi.
Matokeo yaliyoletwa na tume hiyo yakawa asilimia 80 walitaka mfumo wa chama kimoja uendelee huku asilimia 20 wakitamani ujio wa mfumo wa vyama vingi.
Matokeo ya tume hiyo yalimwibua tena Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliyependekeza kuwa msemo wa wengi wape uachwe, badala yake utumike wa wachache wapewe na kusababisha serikali kuruhusu mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, ndipo wapenda mageuzi wakaanzisha vyama vya siasa na kuzoa wanachama kutoka ndani na nje ya CCM.
Wakati huo ndio ambao vijana wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walipojitokeza kujiunga na vyama vya siasa, hasa Chama cha NCCR- Mageuzi kwani ndicho kilichokuwa na nguvu na ushawishi.
Kauli ya Baba wa Taifa iliwafanya NCCR kujipanga zaidi kwani mwaka 1992 walimchagua Mabere Marando kuwa mwenyekiti wa muda NCCR-Mageuzi, kisha 1994 aliidhinishwa rasmi, hivyo ilikuwa ni moja ya hatua za kuendeleza mapambano.
Ilipofika mwaka 1995 baada ya Augustine Mrema, kujiondoa CCM uongozi wa NCCR- Mageuzi ulishauriana kumkaribisha na kumpa uongozi. Lengo la kumkaribisha na kumpa Mrema (sasa marehemu) nafasi ya mwenyekiti wa chama taifa, lilikuwa ni kuongeza nguvu ndani ya NCCR-Mageuzi, huku Marando akiwa katibu mkuu.
Kuanzia 1995 hadi sasa taifa limefanya uchaguzi mkuu mara sita na wa mwakani utakuwa wa saba.
UJIO VYAMA VIPYA
Baada ya kurejeshwa kwa mfumo vya vyama vingi mwaka 1992, uliibuka 'utitiri' wa vyama baadhi yake vikiwa ni NCCR- Mageuzi, TADEA, CUF, CHADEMA, NRA, NLD na DP, UMD na UDP. Vyote vilianzishwa kukabiliana na CCM, lakini vilivyoweka wagombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi, vilikuwa ni vitatu.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 29 mwaka 1995, vyama vya upinzani vilivyoweka wagombea urais vilikuwa ni NCCR Mageuzi (Augustine Mrema) na CUF (Profesa Ibrahim Lipumba).
Chama cha UDP kilimteua John Cheyo kuwania nafasi hiyo, lakini matokeo ni kwamba NCCR- Mageuzi ndicho kilichovizidi vyama vingine vya upinzani kwa kupata wabunge na madiwani wengi.
Hata hivyo, mambo ya siasa yana changamoto zake, baadaye NCCR-Mageuzi ilianza kukumbukwa na migogoro ya kiuongozi ambayo ilisababbisha kikose nguvu hadi leo.
Ni kama kimeshuka kutoka kileleni hadi chini, huku vyama vingine vya CHADEMA na ACT- Wazalendo ambacho sasa kina miaka 10 tangu kianzishwe, kimeendelea kujiimarisha.
Chanzo cha kuimarika kwa chama hicho, ni mgogoro wa uongozi uliotokea CUF na kusababisha wanachama na viongozi kutimkia ACT-Wazalendo na kusababisha CUF nayo kukosa nguvu.
Katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 ya mageuzi, kuna baadhi ya vyama ni kama havipo, ambavyo ni UMD, UDP, DP, NLD, TADEA, NRA, UPDP, TLP, Demokrasia Makini, CHAUSTA na PPT-Maendeleo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED