Utoro huu shuleni unavuruga malengo ya Dira ya 2050

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:00 AM Jan 28 2025
Uvuvi ni shughuli zinazowavutia wanafunzi na kusababisha utoro katika mikoa yenye mito au bahari ama maziwa
Picha: Matandao
Uvuvi ni shughuli zinazowavutia wanafunzi na kusababisha utoro katika mikoa yenye mito au bahari ama maziwa

TANZANIA 2050, inajinasibu kwenye dira yake ya maendeleo, miaka 25 kuanzia leo inatarajiwa kuwa nchi yenye mfumo bora wa elimu katika ngazi zote.

Dira 2050 inasema mfumo huo utajenga maarifa na stadi za wahitimu tena utashabihiana kwa karibu na sekta za uzalishaji ili kuwapatia ajira au kuwawezesha kujiajiri wanafunzi wake.

Inapoanza kuelekea kwenye hatua hiyo nchi ina sera ya serikali kugharamia elimu kuanzia msingi hadi sekondari, lakini kwa uzembe huu wa wazazi na walezi wanaelekea kuikwamisha dira.

Kwa lugha nyingine ni sawa na kusema licha ya serikali kugharamia elimu, kupuuza na kutojali umuhimu wa taaluma ni tatizo.

Mathalani, utoro wa wanaoanza kidato cha kwanza mwaka huu katika baadhi ya maeneo ni kama mfupa ulioshindikana.

Mfano mmojawapo ni huu wa wanafunzi 5,080 kati ya 6,313 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika sekondari za Halmashauri Wilaya Tarime Vijijini mkoani Mara, hawajaripoti shuleni tangu zilipofunguliwa Januari 13, 2025.

Taarifa hiyo inatolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Simion Langoi, katika kikao cha Baraza la Madiwani, wakati wakijadili na kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, wiki iliyopita.

Kaimu mkurugenzi anawaomba madiwani wasaidie kwa kuwa wanafunzi wanaishi maeneo mbalimbali ambayo madiwani hao wapo, na kwamba utoro huo ni aibu kwa halmashauri yao na hata taifa.

Kinachoelezwa na uongozi huo ni mfano mmojawapo kwa mwaka huu wa 2025. Inawezekana kuna maeneo mengine hali ikawa mbaya kuliko sekondari za Tarime Vijijini.

 Kama ndiyo Tanzania inayotaka angalau ikifika mwaka 2050 watoto wawe wamesoma na kufikia elimu ya sekondari, kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, itawezekana?

Hao ni wanafunzi wa shule za sekondari moja lakini  bado hawajatazamwa wa shule za msingi ambao nao wameanza kusoma mwanzoni mwa mwaka. Ikumbukwe tena ni halmashauri moja na cha kujiuliza hali ikoje kwa Tanzania nzima?

Ni suala la kuwafikirisha si madiwani na watendaji wa vijijini, kata, mitaa na vitongoji hata upande wa kutunga sheria nao ni muhimu ufanye jambo ili kukomesha mtindo huo unaokwamisha maendeleo ya elimu.

Kwa kawaida wanafunzi wanatakiwa kuwahi shuleni baada ya mwaka wa masomo kuanza, lakini baadhi yao kama ilivyo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini imekuwa ni tofauti kwani wapo ambao shule inapofunguliwa hawaripoti hadi watafutwe. Inakuwaje mzazi au mlezi?

Imekuwa ni kama mtindo unaoelekea kuzoeleka miongoni mwa jamii kutokana na wanafunzi wachache wa sekondari kuripoti katika shule walizopangiwa huku wengine wakiwa hawajulikani waliko.

Kuna uwezekano baadhi yao wamekwenda katika shule nyingine, lakini ni vyema kuwepo utaratibu wa kueleza mamlaka zinazohusika ili ifahamike. Isionekane kama ni kupuuza masuala ya elimu.

Hata kama watakuwa wamehamia katika shule nyingine, lakini idadi ya watoro wa Tarime Vijijini ni kubwa mno. Kwa idadi hiyo kubwa, ni wazi  huenda wapo walioolewa au kubaki wakifanya kazi za nyumbani.

Lakini wanaohama ni vyema wawe na barua za watendaji wa vijiji au mitaa ili kuweka rekodi za ufuatiliaji watoro, kwani  utoro una athari nyingi ikiwamo kupungua kwa ufaulu, kuongezeka kwa idadi ya raia wasiojua kusoma wala kuandika mbumbumbu hasa ukianzia darasa la kwanza, kuwa na taifa la wasiohitimu na wasio na vyeti hasa  ambao wanaacha shule na hivyo kuathiri maendeleo ya elimu kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa utoro wa wanafunzi hasa wa kidato cha kwanza kila mwaka wa masomo, umekuwa kama jambo la kawaida au ndilo fupa lililoshindikana kutafunwa na fisi na kuachwa libaki kama lilivyo.

Serikali imekuwa ikifanya msako dhidi ya watoro kila shule zinapofunguliwa, ikihusisha kukamata wazazi na walezi, hata hivyo pamoja na juhudi hizo, hali ni ile ile.  

Inaumiza kuona serikali ikipoteza rasilimali hasa kujenga majengo au miundombinu, kuweka watendaji na vitendea kazi lakini inaonekana kama jambo la kawaida hata wanafunzi wasioripoti shuleni na nafasi zao kubaki wazi bila sababu ya msingi bila  maelezo.

Ni muhimu sasa kuangalia upya wapi tatizo lilipo na kuleta ufumbuzi wa kudumu kuliko kuendelea kuwa na hali kama hiyo. Kwani utoro wa wanafunzi shuleni unahitaji kushughulikiwa kwa dhati katika zama hizi za  utawala, uongozi  bora na uwajibikaji kwa maendeleo ya taifa, kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo linalojirudia kila mwaka bila kujua kuwa linaathiri dira na maendeleo ya taifa.

Changamoto hiyo inaweza kushughulikiwa kwa njia ya uwajibikaji na utawala bora kuanzia ngazi ya serikali za mtaa ili kuhakikisha kuwa tatizo hilo linapungua au kumalizika.

Kimsingi, wanafunzi wanaishi katika maeneo mbalimbali ambayo yako chini ya uongozi wa serikali za mitaa. Hivyo, viongozi wa mitaa husika wanapaswa kujua idadi ya wanafunzi waliofaulu na kuwafuatilia.

Kukiwa na mfumo wa kuwafuatilia kuanzia vijijini, vitongojini na serikali za mitaa tangu wanapohitimu na kutangazwa kuingia sekondari, itakuwa rahisi kujua idadi ya  wanaohamishiwa shule nyingine na watoro ili wachukuliwe hatua ili kuepusha nchi kukosa uwezo wa ushindani katika nyanya ya elimu.

Ukweli ni kwamba zipo sababisha pia za nchi kukosa uwezo wa ushindani kwenye nyanya za elimu na teknolojia kwa kuwa wengi hawajasoma, si waelewa wa mambo wala si watafuta maarifa.

Baadhi ya sababu zinazochangia ambazo hutwaja kuchangia utoro kwa baadhi ya wanafunzi shuleni ni umaskini, jamii kutojua umuhimu wa elimu, ndoa za utotoni, kutumikishwa watoto kwenye kazi mashambani, ufugaji na uvuvi, kulelewa na wazee bibi na babu wasio na uwezo wa kufutilia mienendo ya wajukuu wao.

Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022, inaonyesha kuwa mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni na asilimia zake kwenye mabano ni Songwe (45), Ruvuma (37), Katavi (34), Mara (31) na Rukwa (30).

Mara ni mkoa kinara ukiwa kwenye tano bora, hivyo si suala la kufumbiwa macho. Utatuzi wa wake uanze kushughulikiwa kwa njia ya uwajibikaji, viongozi wa serikali za mitaa walisimamie kwa nguvu zao zote ili lipungue au kumalizika.