Timu tano zilizoshangaza mashabiki Ligi Kuu Bara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:41 PM Jan 06 2025
Kikosi cha Tabora United  kabla ya kucheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Novemba 7, mwaka jana na kushinda mabao 3-1
Picha: Mtandao
Kikosi cha Tabora United kabla ya kucheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Novemba 7, mwaka jana na kushinda mabao 3-1

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu unaanza, mashabiki wengi wa soka nchini walizitabiria timu nne, Simba, Yanga, Azam na hata Singida Black Stars kufanya vema. Na kweli, hadi mzunguko wa kwanza unamalizika zimefuatana kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Simba inaongoza ikiwa na pointi 40, ikiiacha Yanga kwa pointi moja tu, inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 39. Azam ni ya tatu ikiwa na pointi 36, huku Singida Black Stars ikikalia nafasi ya nne na pointi zake 33.

Baada ya hapo kuna timu ambazo zina mazoea ya kutikisa maeneo ya kati ya ligi kila msimu, mfano msimu uliopita Coastal Union ikifanya hivyo hadi kufanikiwa kucheza Kombe la Shirikisho Afrika, KMC, Kagera Sugar na zingine.

Hata hivyo, msimu huu umekuwa tofauti. Hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza kuna timu ambazo zimeonekana kuwa tishio kwenye Ligi Kuu na kushangaza mashabiki wengi kutokana na si tu kuwa sehemu nzuri kwenye msimamo wa ligi, bali hata upinzani zinaoutoa, tofauti na msimu uliopita ambapo baadhi yake ziliponea chupuchupu kushuka daraja, zingine zikiponea kwenye 'play off.' Hebu tuziangalie timu hizo, kazi zilizozifanya hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza...

1# Tabora United

Imekuwa ni moja kati ya timu tishio kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na kushangaza wengi. Ndiyo timu iliyowafunga Mabingwa Watetezi, Yanga mabao 3-1, ikifanya hivyo Novemba 7, mwaka jana, Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam, kwenye mchezo wa ligi na kuwaacha wengi midomo wazi.

Si jambo la kawaida kwa timu kubwa za Simba na Yanga kufungwa idadi kubwa ya mabao kama hayo na timu za daraja la kati kama hiyo.

Ikaifunga pia, Azam mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa, Desemba 13, mwaka jana, ikiwa nyumbani, na kuilazimisha sare ya mabao 2-2, Singida Black Stars, ambayo ilikuwa inaongoza mabao 2-0 hadi kipindi cha pili.

Ni timu ambayo haikutarajiwa kufanya maajabu hayo hadi mzunguko wa kwanza kwani msimu uliopita, ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya 14 na kucheza mechi ya mchujo dhidi ya JKT Tanzania, ikachapwa mabao 4-0 nyumbani, kabla ya kulazimisha sare ugenini, kiasi cha kulazimika kwenda kucheza 'play off' ya pili dhidi ya Biashara United iliyotoka Ligi ya Champioship.

Ililazimika kushinda mabao 2-0 nyumbani, baada ya kupoteza bao 1-0 ugenini, na kupata ushindi wa jumla wa mabao 2-1 ulioibakisha Ligi Kuu. Hadi inamaliza mzunguko wa kwanza msimu huu, ipo nafasi ya tano nyuma ya Singida Black Stars, ikiwa na ponti 25.

2# Mashujaa FC

Huu ni msimu wa pili inacheza Ligi Kuu Tanzania Bara. Msimu uliopita pamoja na kuanza vizuri michezo ya mwanzo, ilianza kufanya vibaya kwenye mechi nyingi zilizofuatia kiasi cha kudhaniwa kuwa inaweza kushuka daraja.

Ushindi wa michezo mitatu mfululizo ya mwisho, na ule wa mwisho dhidi ya Dodoma Jiji ilioshinda mabao 3-0 uliifanya kufikisha pointi 35 na kushika nafasi ya nane kwenye msimamo, ikikwepa kwenda 'play off', ikisaidiwa pia na matokeo ya michezo mingine ya kumaliza msimu ilioicha salama.

Haikudhaniwa kuwa mpaka mzunguko wa kwanza msimu huu inaweza kuwa 'ngangari', kwani ipo nafasi ya saba, ikiwa na pointi 19 kwa michezo 16 iliyocheza.

3# JKT Tanzania

Ni moja kati ya timu ambazo nusura ziteremke daraja mwaka jana. Mechi ya mwisho ya kumaliza msimu ilikutana na kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Simba, Mei 28, mwaka jana.

Kipigo hicho kiliifanya kumaliza nafasi ya 13 kwenye msimamo ikimaliza ligi na pointi 32, ikamalizika kwenda kucheza mechi ya mchujo na Tabora United iliyomaliza nafasi ya 14.

Kwa bahati nzuri ilishinda mabao 4-0 ikiwa ugenini, Ali Hassan Mwinyi, Tabora na kulazimika 'kushikilia bomba' kwenye mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ililazimisa suluhu ambayo iliibakisha Ligi Kuu.

Mpaka kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, imekuwa moja kati timu sumbufu kwenye Ligi Kuu.

Msimu uliopita ilifungwa mabao 5-0 na Yanga mzunguko wa kwanza, lakini huu ilifungwa mabao 2-0, ikicheza ikiwa pungufu, huku kipa wake namba moja akiwa amepigwa kadi nyekundu, ikatoka suluhu dhidi ya Azam, mechi ya mzunguko wa kwanza, sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida Black Stars na kufungwa kwa taabu, dakika za majeruhi dhidi ya Simba, Desemba 24 mwaka jana.

Iko nafasi ya nane ya msimamo ikiwa imecheza mechi 16 na kukusanya pointi zake 19 mpaka sasa.

4# Fountain Gate

Ilionekana na mashabiki wengi wa soka nchini kama imefanya usajili wa kuungaunga. Ikumbukwe kuwa hii ndiyo ilikuwa Singida Big Stars ambayo wachezaji wake wengi mahiri walipelekwa kwenye timu ya Ihefu FC ya Mbarali, Mbeya.

Baadaye Ihefu ikiwa na wachezaji wengi wa Singida Big Stars, ilihamia Singida na ikabadilishwa jina ikawa Singida Black Stars, huku iliyobaki nayo ikaamuwa kujibadilisha jina na kuwa Fountain Gate, na maskani yake yakatoka Singida na kwenda mkoani Manyara.

Kutokana na kuchukuliwa na wachezaji wengi tegemeo, Fountain Gate haikutegemea kufanya lolote mpaka mzunguko wa kwanza kwani ilibaki bila kusajili wachezaji wenye majina makubwa au wengi kutoka nje ya nchi.

Kwa namna ya kushangaza ilianza Ligi Kuu kwa kishindo ambapo kuna wakati ilikuwa ikiongoza ligi hiyo.

Ni moja kati ya timu nne zilizofunga ambao mengi kwenye Ligi Kuu, ikiwa imepachika 24. Mastraika wake , Selemani Mwalimu mwenye mabao sita, na Edgar William aliyepachika mabao matano, wakiwa kwenye orodha ya wanaowania kiatu cha dhahabu. Yenyewe ipo nafasi ya sita kwenye msimamo ikiwa na pointi 20.

5# Dodoma Jiji

Inakamata nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, ikikusanya jumla ya pointi 19.

baada ya kutofanya vema kwa misimu miwili mfululizo, hakuna aliyetarajia kuwa ingeweza kuwa hapo ilipo mpaka sasa.

Msimu uliopita ilimaliza ikiwa nafasi ya 12, ikiwa na pointi 33, pointi moja tu juu ya JKT Tanzania iliyokwenda kucheza 'play off' na Tabora United.

Pamoja na kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo wa mwisho, ilipona kwenda kucheza 'play off' kwa kuokolewa na Simba, iliyoifunga JKT Tanzania mabao 2-0 katika mchezo wa mwisho na kuibakisha ikiwa na pointi 32 iliyoilazimu kwenda kwenye mchujo na kuiacha Dodoma Jiji ikipeta.