WAPENZI wa chai ya rangi wanafurahia ile nyeusi ambayo imezoeleka karibu kila mahali, lakini sasa Bodi ya Chai Tanzania (TBT), inapania kuleta chai ya kijani yenye ladha tofauti na bora kiafya.
TBT inaongeza vionjo kwenye chai kwa kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ili pamoja na ladha na ubora inakusudia kuiwezesha chai ya Tanzania kutawala soko la kitaifa na kimataifa.
Ni hatua inayofanikishwa baada ya ziara ya kampuni mbili zinazowekeza kwenye chai kutoka Japan ziara inayowezesha pande mbili hizo kukubaliana kubadilishana ujuzi na namna ya kutumia teknolojia ya kisasa kuongeza chai.
Wajapani hao wanaonyesha teknolojia ya kutengeneza chai ya kijani na vifungashio bora zaidi jambo linaloikuna TBT inayoanza kuweka mipango ya kutumia teknolojia ya kisasa ikiamini italeta mapinduzi ya viwanda.
Katika video fupi Wajapani wanaonyesha namna wanavyotumia mitambo mbalimbali na mashine kulima na kuchakata chai, kuanzia shambani mpaka kiwandani kisha kumfikishia mlaji hatua ambayo ni somo kwa bodi.
Hii ni sawa na kusema, ziara iliyofanywa na TBT Japan nchini Japan Julai mwaka huu imeleta matokeo chanya kwa kufanikisha kushawishi kampuni za Kawasaki Kiko na Nasa Corporation, ambazo mbali na kubadilishana ujuzi zimefunza wakulima mengi kuhusu kilimo cha zao hilo.
Ni baada ya kutembelea baadhi ya mashamba yaliyoko Iringa na Njombe zikiwamwagia sifa wakulima na chai ya Tanzania kuwa inafaa pia kuzalishwa chai ya kijani badala ya nyeusi ambayo ndiyo majani yanayotumika nchini.
Ugeni huo, ukiwa mkoani Njombe unatembelea shamba la Kibena pamoja na kiwanda cha Lipton, mashamba ya Chama cha Ushirika cha Mkonge Mufindi na kuzungumza na wakulima.
Wageni kutoka Japan wakiongozana na baadhi ya viongozi kutoka Bodi ya Chai -Kaimu Mkurugenzi wa bodi, Beatrice Banzi pamoja na wataalamu wa Wizara ya Kilimo, kwa nyakati zote wageni hao, walionyesha kufurahishwa na namna zao hilo linavyolimwa kwa wingi nchini.
Katika Kituo cha Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT) wanafurahia uwezo mkubwa wa utafiti wa kituo hicho ambapo kimefanya tafiti na kuzalisha majani ya chai yaliyowavutia kwa kuwa yanafaa katika uzalishaji wa chai ya kijani.
Wanasifu kuwa chai ya Tanzania ni bora na wameona yenye majani membamba ambayo ndio inahitajika zaidi Japan kwa ajili ya kutengeneza chai ya kijani.
Aidha, mitambo wanayoliyonayo inawezakuchakata majani membamba, hata mapana nayo ni ya kisasa nasifu … akiwa ameshika jani la chai akitabasamu kwa bashasha.
Anawasihi wakulima waendelea kufanya uwekezaji katika chai ya majani membamba na kwamba ina soko kubwa Japan.
WAPIMA CHAI
Wakati wanakagua chai katika maeneo hayo, waliipima kwa kutumia tepu kwa lengo la kulinganisha na mashine zao ili kuona kama ukubwa au udogo wake hautaathiri mashine zao wakati wa kuchakata.
Aidha walilenga kuona namna ya kutengeneza mashine za kuchakata chai hiyo zitakazoendana na uhalisisa wa chai inayozalishwa nchini.
Beatrice Banzi kutoka TBT anasema ziara hiyo imekuwa ya mafanikio kwa kuwa Wajapan wamejionea mafanikio makubwa katika sekta hiyo.
Beatrice ambaye anawapitisha wageni hao kwa hatua kwa hatua katika mashamba na viwanda, anasema kampuni hizo ni kubwa na ni wazi zitaleta matokeo chanya katika kukuza zao hilo.
Awali akiupokea ugeni huo katika ofisi za bodi hiyo jijini Dar es Salaam anasema matarajio yao baada ya ziara hiyo ni kufanya mapinduzi makubwa ya viwanda.
"Tumeona wanasema hawana nguvu kazi ndipo wakaanza kubuni jinsi ya kufanya kazi za shambani bila watu kwa kutumia mapinduzi ya viwanda.
"Na sisi tunachokitarajia, ni mapinduzi ya viwanda kwa sababu wao hawana nguvu kazi sisi tunayo, lakini mitaji ya kuwalipa inakuwa shida kwa hiyo ni vizuri kutumia viwanda vyenye teknolojia ya kisasa ambavyo vitasaidia kupunguza gharama katika uzalishaji wa chai kama wanavyofanya wao," anasema Beatrice.
Anaongeza mbali na mapinduzi ya viwanda pia ni kuongeza ubora wa chai inayozalishwa nchini ili kulitawala soko la ndani na nje pia.
Ofisa Kilimo Idara ya Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo, Bahati Majaliwa, anasema mpango wa serikali ni kujenga viwanda vidogo vidogo vitakavyo wasaidia wakulima kusindika chai ili waweze kupata faida zaidi kutokana na mauzo.
"Wajapan wameipenda sana chai yenye majani membamba, na inazalishwa kwa wingi, katika maeneo mengi ya uzalishaji hapa nchini zaidi ya asilimia 80 ya chai hiyo inazalishwa.
"Wakulima waendelee kutunza mashamba yao vizuri ili kupata tija kutokana na majani watakayozalisha," anasema Majaliwa.
Mkakati wa Wizara ya Kilimo kwa sasa ni wakulima kusindika chai yao na kwamba mpango uliopo ni kuwekeza katika viwanda vya wakulima wadogo.
Anasema ujenzi wa viwanda kwa wakulima wadogo utawainua kiuchumi na kuzalisha chai yenye tija itakayoleta ushindani katika soko la kitaifa na kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT), Dk. Daniel Mgori, anasema hatua ya ugeni huo kutembelea katika kituo chao umewapa somo na kujua aina ya chai inayohitajika Japan.
Hapa Dk. Mgori, anawahakikishia Wajapan Wizara ya Kilimo, na Bodi ya Chai kwamba taasisi hiyo itafanya jitihada za kuzalisha kwa wingi miche yenye majani membamba ili wakulima waweze kulikamata soko lao.
Anasifu kampuni zilizowatembelea zimeongozana na wataalamu wa kutengeza mashine za kuchakata chai na wamewapa ushauri wa namna ya kulima zao hilo.
Mwenyekiti wa Mashamba ya Chama cha Ushirika cha Mkonge, Balodaniel Mgonzo aliuomba ugeni huo, na serikali, kuwajengea kiwanda ili waachane na adha ya kuuza majani mabichi jambo linalowasababishia hasara.
Kufanikisha hilo, Mgonzo anasema tayari wametenga kiwanja chenye ukubwa wa hekari 12 ili atakapopatikana mwekezaji awajengee kiwanda waweze kuuza majani makavu.
Anasema wanakabiliana na changamoto ya malipo kidogo, ukilinganishwa na gharama za uendeshaji wa mashamba.
"Tunawakaribisha Wajapan waliokuja kututembelea leo, wajenge viwanda wanavyotaka na kama eneo tulilotenga halitatosha kuna sehemu jirani ya wakulima wapo tayari kujitolea," anasema Mgonzo.
Meneja Masoko TBT, Selemani Chillo, anawatoa shaka wakulima kwamba hali ya masoko ya chai nchini inazidi kuimarika na tayari wameshafungua masoko katika nchi za Omani, Sudan, na sasa mkakati walionao ni kufungua mengine katika nchi za Kiarabu.
Selemani anasema walipokwenda Japan waliwashawishi kuja nchini kuangalia fursa mbalimbali za chai, na kujifunza kutoka kwao teknolojia wanayoitumia iweze kutumika nchini katika kuongeza thamani ya chai na soko.
WAWEKEZAJI WAITWA
Wakati huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao, Dk. Hussein Omar, anawataka wawekezaji kujitokeza kuwekeza kwenye sekta ya chai kuiinua ili achangie pato la taifa.
Dk. Omar anasema iwapo wawekezaji watajitokeza kwa wingi zaidi kuwekeza kwenye mnyororo mzima wa chai hususan katika kufungua viwanda vya uchakataji na ufungashaji wakulima wengi wa chai watanufaika.
Anasema, sekta ya chai ina fursa lukuki na zote hizi zinaweza kuiinua hivyo ni imani ya wizara kuwa kampuni za Japan kwa kuwa ni za uchakataji na ufungaji zikinunua moja kwa moja chai za wakulima watakuwa na soko la uhakika na wigo mpana zaidi wa kuuza zao hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED