Samia vitani; anaingiza darasani Bil. 10/- kila mwaka, zimrejeshee mabingwa 30

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 09:19 AM May 09 2024
Ndivyo ilivyo, tukio mojawapo la Mwezi wa Uelimishaji Saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dar es Salaam.
Picha: Maktaba
Ndivyo ilivyo, tukio mojawapo la Mwezi wa Uelimishaji Saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dar es Salaam.

KUNA shida katika kuongezeka idadi ya wagonjwa wa saratani kila mwaka. Idadi ya wanaobainika kila mwaka ni 40,000 na wanaofariki ni 27,000.

Ni tahadhari inayoleta nakisi inayoongeza idadi ya wagonjwa wa kansa, 13,000 kila mwaka. Hapo inamshtua Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika vita vyake, oneo hilo la kuumba wabobezi na wabobevu wa kupambana nayo.

 Kujibu tishio hilo, Rais Dk. Samia anatoa ofa ya ’kuwaumba’ mabingwa 30 kila mwaka, Waziri wa Afya. Dk.Ummy Mwalimu, akiwa na ufafanuzi: “ Dk. Samia Super-Specialized scholarship Programme imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi ambapo kwa mwaka wa masomo 2023/2024.

 “Jumla ya shilingi bilioni 10.9 zimetengwa na kuwawezesha wanafunzi 1,109 kwenye masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi (30 ni wa saratani).” 

 Kimsingi, Rais Dk. Samia alishafafanua utashi na ushiriki wake katikia vita hivyo miaka sita iliyopita, akiwa Makamu wa Rais, kwamba ukishafikia kwa karibu familia yake.

 Hiyo ilikuwa katika uzinduzi wa kampeni vita dhidi ya Saratani ya Mlango wa Kizazi,  inayoongoza kwa kuua, kati ya saratani zote, ikiwa tukio la uzinduzi wa chanjo dhidi yake, katika viwanja vya Mbagala Zalheim, Aprili 2018, akitamka: “saratani hii ndiyo iliyomwondoa mama yangu kipenzi.

 Mtendaji wake wizarani, Ummy, hadi sasa bado ziko aina nyingi za saratani zinazochukua maisha ya wengi nchini na kwa jumla ya vifo vote, saratani ya mlango wa kizazi ina asilimia 25 ya wote wanaougua saratani, ikifuatiwa na saratani ya matiti yenye asilimia 10.

 Ilikuwa kwenye uzinduzi wa Jengo la Huduma za Saratani, katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, lenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa 100 kwa siku, mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dk. Doto Biteko, wiki iliyopita.  

 Kuhusu mwelekeo wa hali ya saratani nchini, Ummy ana ufafanuzi wa kiserikali:“Vifo vitokanavyo na saratani vitaongezeka ifikapo mwaka 2030, kama hatutachukua hatua za kushughulikia ukubwa wa tatizo hili la saratani nchini, inakadiriwa kufika vifo milioni moja.” 

 VITA VILIVYOKO

Waziri anasema, serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na mapambano dhidi ya saratani, kwamba fedha zimepatikana za kuboresha miundombinu, ununuzi wa vifaa vya kisasa na kusomesha wataalamu katika matibabu ya saratani (mabingwa 30 kila mwaka). 

 Akifungua Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani Tanzania (APHYTA) katika ukumbi wa Kinataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, akanena mwaka huu idadi ya madaktari wanaojiendeleza, kuna ziada ya 582, kulinganisha na mwaka uliopita wa masomo.

 Anafafanua wanafunzi 79 watasomea udaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na kati yao, madaktari 11 sawa na asilimia 33, wameenda kusoma ubingwa bobezi wa magonjwa ya ndani.

 Hapo Waziri Ummy anatoa wito kwa madaktari vijana wajitokeze kwa wingi kujiendeleza katika masomo ya ubingwa na ubobezi na wakirudi, wawe tayari kupangiwa vituo vya kazi sehemu yoyote kitaifa, wanakohitajiwa. 

 “Kupitia muundo huu mpya wa Sekta ya Afya, tutaweza kuwatambua kwa kuwawekea mazingira mazuri madaktari wenye ubobezi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo wa masuala ya magonjwa ya ndani,” anasema.

 Katika mkutano huo, Waziri Ummy akawataka madaktari hao kujadiliana, wao wizarani wapate mapendekezo ya jinsi ya kupunguza magonjwa yasiyoambukiza, kwa kuwa sasa kuna kasi ya ongezeko lake. 

 Vilevile, Waziri Ummy akawataka madaktari hao kujadiliana na kutoa maoni yao katika mwongozo sahihi wa kitaifa wa matibabu, pamoja na orodha ya taifa ya dawa, ili penye mapungufu yarekebishwa. 

 “Suala la ‘Kitita cha Bima ya Afya NHIF’ linatakiwa lijadiliwe kuanzia kwenye mwongozo wa kitaifa wa matibabu, pamoja na orodha ya Taifa ya dawa, tukishakubaliana, tunamwambia NHIF atambue na afuate mabadiliko hayo,” anasema.