"WAMENIAMBIA mambo yako mama eee, wamenieleza matatizo ya mume wako eee, ya kisa cha wewe sheri Zinduna, kufika kupewa talaka." Ni mwanzo wa wimbo uliotungwa na gwiji la muziki Tanzania, Zahir Ally Zorro. Ikumbukwe kuwa mwanamuziki huyu ndiye baba wa mwanamuziki Banana Zorro.
Ni wimbo ambao una kisa kimoja cha ajabu na kusikitisha sana. Nimeamua kuja na mada hii leo ili tuangalia jinsi wanamuziki wa zamani walivyokuwa na uwezo wa kuchua visa vya kweli kabisa na kuviweka kwenye muziki, vikafundisha, kuelimisha, kufurahisha na kufikirisha watu.
Hiki ni kisa cha ukweli kabisa kilichotokea kwenye miaka ya 1980.
Ni kisa cha picha iliyopigwa zamani katikati ya jiji la Dar es Salaam, lakini ikaenda kuvunja ndoa miaka mingi baadaye jijini Mwanza. Hebu tuendelee na mashairi ya wimbo huu.
"Photo albamu inaleta maneno, katikati ya jiji la Mwanza, kisa ni picha iliopigwa zamani, katikati ya Dar es Salaam. Sheri Zinduna nakupa pole Zinduna. Matatizo yanayokukuta. Mkasa nyumbani kwako, ndoa imevunjika, kisa ni picha ya zamani ooo. Afadhali kama mimi ningewahi kufika Mwanza, lakini tangu mimi nimezaliwa, sijafika Mwanza ooo. Vitongoji vya Namanyoro, Kirumba na Mtaa wa Sukuma, nimeelezwa na wenyeji ooo." Hapa ndipo wimbo huo ulipokamilika.
Maudhui ya wimbo huu, ni kwamba huyu dada Zinduna aliolewa na jamaa jijini Mwanza. Lakini kabla ya kuolewa alikuwa na mpenzi wake. Waliwahi kupiga picha katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Mwanadada huyo inaonekana alihifadhi picha hiyo sehemu ambayo anaijua yeye hata baada ya kuachana na mpenzi wake huyo na kupata mchumba ambaye alikuja kumuoa, akawa mumewe.
Baada ya kuolewa, makazi ya Zinduna na mumewe yakahamia jijini Mwanza kutoka Dar es Salaam.
Kilichotokea baada ya miaka michache, mume wa Zinduna aliifuma picha ya mkewe aliyopiga na mpenzi wake katikati ya jiji la Dar es Salaam. Sijui ilikuwaje, lakini aliifuma picha hiyo iliyofichwa vizuri kwenye 'photo albamu'.
Mume alichanganyikiwa, na kwa bahati mbaya sana ni kwamba gauni alilovaa Zinduna lilifanana sana na lile alilomnunulia siku chache zilizopita.
Mume akiangalia anaona ni kama picha ya zamani ambayo haikupigwa Mwanza, lakini hayo yote yanamezwa na gauni hilo alilomnunulia hivi karibuni. Akawa anajiuliza kama ni picha ya zamani, mbona gauni hili ndiyo hilo alilomnunulia majuzi. Kwa hiyo akadhani kabisa kuwa picha hiyo haikupigwa siku nyingi. Kwa hiyo akaona kabisa kuwa kumbe mkewe anamsaliti.
Pamoja na Zinduna kujitetea kwa anavyojua kuwa picha hiyo ni ya mpenzi wake wa zamani, miaka zaidi ya kumi iliyopita kabla hata ya kukutana na yeye, tena ilipigwa Dar es Salaam, mume hakukubali. Kilichofuata ni talaka. Zinduna alilia na kusononeka. Akarejea kwao Dar es Salaam.
Mpenzi wa zamani ambaye alipiga naye hiyo picha akasikia habari hizo. Alisikitika sana na hakujua afanye nini ili amsaidie, kwani naye alikuwa ameshaoa. Basi akabaki na yeye analalamika na kumpa pole mpenzi wake wa zamani Zinduna.
Anayesikika anaimba kwenye wimbo huo kwa jinsi ulivyopangiliwa, ndiye mpenzi wa zamani wa Zinduna, anamwambia wameniambia mambo yake na matatizo yake na kisa cha mpenzi wake wa zamani Zinduna kufika kupewa talaka, kisa ni 'photo albamu' iliyokuwa na picha waliopiga zamani katikati ya Dar es Salaam, ikaleta maneno jijini Mwanza.
"Alipaswa baba watoto ajue, sijawahi kufika Mwanza, toka mimi nizaliwa, sijafika Mwanza." Jamaa anamfariji mpenzi wake wa zamani, kuwa mumewe alipaswa ajue kuwa yeye hajawahi kufika Mwanza tangu azaliwe, hivyo hiyo picha siyo ya hivi karibuni, bali ya zamani kabla hajaolewa. Kama angewahi kufika Mwanza, basi angeweza kuwa na wasiwasi kuwa amepiga picha na mkewe, lakini vitongoji vyote anavisikia kwa watu.
Wimbo huu uikumbusha jamii kuwa kuna wakati watu wanafanya maamuzi makali na magumu kwa vitu ambavyo hawajavifanyia utafiti wa kutosha, au kufanya upepelezi, bali ni hasira na mihemko.
Ni kwamba inafaa kwanza kabla ya kuamua jambo lolote hasa lenye mustakabali wa maisha yetu ni lazima tujiridhishe kwanza. Zinduna amepewa talaka kwa kosa ambalo hajalifanya. Na mumewe kama alikuja kujua hilo baadaye anaweza kumshawishi mkewe warudiane? Na kama akikataa kuna kosa?
Meseji namba: 0716-350534
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED