DONALD Trump ametia saini maagizo kadhaa baada ya kurejea katika kiti cha uongozi wa Marekani, huku akiahidi kuchukua hatua za haraka katika baadhi ya ahadi alizotoa wakati wa kampeni.
Miongoni mwa maagizo ambayo yamevutia umma ni ukandamizaji wa wahamiaji na kuziondoa baadhi ya sera nzuri za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hatahivyo uwezo wake una kikomo kwa sasa, anakabiliwa na vikwazo kabla ya mipango yake kuidhinishwa.
Hapa kuna hatua sita za kuvutia zilizochukuliwa na Trump.
KUTANGAZA GENGE LA DAWA ZA KULEVYA
Amesema yatatangazwa magenge ya dawa za kulevya kuwa 'mashirika ya kigaidi ya kigeni'
Agizo hilo linasema kuwa magenge "yamejihusisha katika kampeni za vurugu na ugaidi" duniani katika kuijaza Marekani na uhalifu, na kusababisha hatari ya usalama wa taifa kwa Marekani.
Zaidi ya hayo, agizo hilo linabainisha kuwa sera ya Marekani ni "kuhakikisha kuangamizwa" kwa makundi haya nchini Marekani.
Inayapa mashirika ya Marekani siku 14 kutoa mapendekezo kuhusu ni vikundi vipi vitaangaziwa na kuwa tayari kuharakisha kuondolewa kwa watu binafsi kutoka Marekani.
Kulitaja kundi moja kuwa la kigaidi kunaweza kufungua milango ya kuwafungulia mashitaka raia wa Marekani au hata biashara halali zitakazopatikana kuwa na uhusiano na makundi hayo.
Utambuzi huo pia unaweza kuzorotesha uhusiano na nchi ikiwemo Mexico, ambayo imetoa wito kwa uhuru wake kuheshimiwa.
Utambuzi wa vikundi hivi kuwa mashirika ya kigeni ya kigaidi unaweza hatimaye kutumiwa kuhalalisha hatua za kijeshi dhidi ya walengwa nchini Mexico au nchi zingine ambazo vikundi kama hivyo vinafanya kazi.
Utambuzi huo pia unaweza kufanya serikali ya Marekani kutoa rasilimali zaidi na zana za kisheria zilizoimarishwa, ili kupigana na vikundi na magenge mengine na kufuatilia masilahi yao ya kibiashara na kifedha katika pande zote za mpaka.
Ingawa inaweza kufanya "msaada wa nyenzo" wa vikundi hivi kuwa uhalifu, bado haijulikani ni nini inaweza kumaanisha.
Kinadharia, hiyo inaweza kumaanisha kuwa wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya, wakiwemo raia wa Marekani, wanaweza kushtakiwa kwa kuwasaidia magaidi - mbali na raia wa Marekani au wafanyabiashara walioko kwenye mpaka wanaolazimika kuwalipa.
KUJIONDOA MKATABA WA PARIS
Agizo hilo linamtaka balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa "mara moja" kuwasilisha ombi rasmi la maandishi la kujiondoa kwenye makubaliano ya hali ya hewa ya Paris.
Linasema mkataba huo hauakisi maadili ya nchi au malengo yake ya kiuchumi na kimazingira
Nchi yoyote inaweza kujiondoa katika mkataba wa mabadiliko ya tabianchi duniani, lakini kanuni za Umoja wa Mataifa zinasema kuna mchakato wa kuondoa nchi unaofuatwa.
Trump alitangaza nia yake ya kujiondoa katika muhula wake wa mwisho mwaka wa 2017, lakini mpango huo haikukamilishwa rasmi hadi 2020. Tunaweza kutarajia kipindi kingine cha kusubiri kwa angalau mwaka mmoja.
Rais Joe Biden, aliirudisha nchi hiyo kwa WHO muda mfupi baada ya kuchukua madaraka mnamo 2021.
Marekani inawajibika kwa karibu 11% ya uzalishaji wa gesi chafu duniani, na kuifanya kuwa mchafuzi wa pili kwa ukubwa nyuma ya Uchina. Hii inaharibu juhudi za kimataifa za kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Kujiondoa kwake huko kumeibua masuala ya uaminifu juu ya uongozi wa hali ya hewa, na maswali kuhusu iwapo makubaliano yenyewe yamekuwa na ufanisi.
Kujiondoa huko pia kunaendana na lengo la Trump la kuongeza uzalishaji wa mafuta na gesi ndani ya nchi, ingawa Marekani tayari ndiyo nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa zote mbili duniani. Ni mojawapo ya mabadiliko kadhaa ya Trump ya ulinzi wa mazingira ambayo yalipitishwa na utawala wa Biden.
KUKOMESHA URAIA WA KUZALIWA
Agizo hili linalenga kukomesha uraia wa haki ya kuzaliwa kwa watoto waliozaliwa Marekani, kwa wazazi wahamiaji ambao wako nchini kinyume cha sheria, pamoja na wale waliozaliwa na wazazi ambao wako nchini kwa muda mfupi.
Kumekuwa na ripoti kwamba uongozi utatekeleza agizo hilo kwa kuzuia hati, kama vile pasipoti, kutoka kwa watu ambao inawaona kuwa hawastahiki uraia.
Kanuni ya uraia wa kuzaliwa imeanzishwa katika Katiba ya Marekani. Marekebisho ya 14 yanasema kwamba "watu wote waliozaliwa au walio na asili ya nchini Marekani" ni raia wa Marekani.
Changamoto za kisheria tayari zinaendelea - mtu mmoja anadai agizo hilo "ni kinyume cha katiba, na linakiuka maadili ya kimsingi ya Kimarekani".
"Hatimaye hili litaamuliwa na mahakama. Hili si jambo ambalo [Trump] anaweza kuamua mwenyewe," Saikrishna Prakash, mtaalamu wa masuala ya katiba, aliiambia BBC.
Trump ametishia kuwafukuza watu wengi, ikiwemo wale ambao uraia wao wa kuzaliwa utaondolewa ikiwa Trump atafanikiwa kutekeleza hatua hii.
Kesi za kisheria hatimaye zinaweza kuamuliwa na Mahakama ya Juu ya Marekani, ambayo inaweza kuchukua muda mrefu.
KUIONDOA MAREKANI WHO
Agizo hilo linasema Marekani ilikuwa ikijiondoa "kwa sababu ya shirika hilo kutoshughulikia janga la Covid-19" inavyostahili
Chuki ya muda mrefu ya Trump dhidi ya WHO inatokana na dhana kwamba Uchina inapendelewa na shirika hilo , na kwamba taifa hilo kwa mujibu wa Trump lilihusika na kuenea kwa virusi vya maradhi hayo.
Pia inataja "ufadhili wa kutaabisha usio wa haki" ambao Marekani inatoa kwa WHO.
Ni mara ya pili kwa Trump kuamuru Marekani iondolewe kwenye WHO. Alianza mchakato huo na baadaye Biden akabatilisha uamuzi huo baada ya kuchukua wadhifa huo.
Kujiondoa kwa Marekani hakutaanza kutekelezwa hadi mapema 2026 , lakini kuondoka kutahitaji idhini ya bunge la Congress.
Kwenye karatasi, Warepublican wana wabunge wengi katika mabunge yote mawili ya Congress. Lakini idadi yao ni ndogo, na ingewachukua wapinzani wachache tu wa Republican kuzuia uwezekano wa kuondoka.
"Janga!", ni jibu la baadhi ya wataalam wa afya ya umma duniani wanavyoielezea.
Kati ya nchi wanachama 196, Marekani ndiyo nchi inayotoa mchango mkubwa, ikichangia karibu asilimia tano ya bajeti yote ya WHO.
Inawezekana kwamba ufadhili unaweza kusitishwa mara moja na hiyo inaweza kuwa na athari kwa uwezo wa WHO kukabiliana na masuala ya dharura.
Pia kuna wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wanasayansi kwamba hatua hiyo itaiwacha Marekani ikiwa imetengwa linapokuja suala la upatikanaji wa programu kama vile kujitayarisha kwa janga na mpangilio wa msimu wa mafua, ambao hutumiwa kukuza chanjo za mafua za kila mwaka.
Hiyo inaweza hatimaye kudhuru afya ya Wamarekani, na maslahi ya kitaifa ya Marekani.
Baadhi wanahoji kujiondoa kwa Marekani kunaweza kusababisha mageuzi zaidi ya jinsi WHO itakavyofanya kazi, na kuifanya kuwa chombo kinachohudumia vyema mahitaji ya afya ya umma ya watu kote duniani.
KUBADILISHA JINA LA GHUBA YA MEXICO
Agizo hilo linataka Ghuba ya Mexico "ibadilishwe rasmi na kuitwa Ghuba ya Amerika".
Trump anaweza kubadilisha jina la Ghuba kwenye nyaraka rasmi za serikali ya Marekani.
Hili limetokea kwenye baadhi ya hati za Marekani - ikiwa ni pamoja na habari za hali ya hewa kutoka kwa Gavana wa Republican huko Florida Ron DeSantis, ambayo inarejelea "eneo la shinikizo la chini linalovuka Ghuba ya Amerika".
Trump hawezi kulazimisha nchi au makampuni mengine kubadili jina.
Kwa mfano, kwa sasa Ghuba hiyo inasalia na jina la Mexico kwenye ramani za Google.
Hakuna makubaliano rasmi ya kimataifa ya kutaja maeneo ya baharini - ingawa kuna chombo ambacho kinataka kusuluhisha mizozo ikiwa itatolewa.
Kwa hivyo Mexico inaweza kuibua mzozo rasmi, na washirika wa Amerika na Mexico wanaweza kujipata katika mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Katika kujibu agizo hilo, Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum alisema Marekani inaweza kuiita "Ghuba ya Amerika", lakini hii haitabadilisha jina linalotumiwa na Mexico na dunia nzima.
MAREKANI KUTAMBUA JINSI MBILI PEKEE, WANAUME NA WANAWAKE
"Ni sera ya Marekani kutambua jinsi mbili, wanaume na wanawake. Jinsia hizi hazibadiliki na zimewekwa katika ukweli wa kimsingi na usiopingika," inasema, na kuongeza kuwa serikali ya shirikisho itatumia neno uke au uume, sio utambulisho wa kijinsi.
Timu ya Rais Trump inahoji kwamba mahitaji ya kurejelea watu waliobadili jinsia katika vituo vya serikali na maeneo ya kazi kwa kutumia matamshi yanayolingana na utambulisho wao wa kijinsia yanakiuka Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani kuhusu uhuru wa kujieleza na wa dini.
Mataifa kama Kansas na Montana tayari yametunga sheria ya kuweka ufafanuzi wa kibayolojia wa uume au uke kuwa sheria.
Kuna uwezekano wa kuwa na changamoto za kisheria.
Kampeni ya Haki za Kibinadamu, ambayo inawakilisha watu wa LGBTQ+, ilisema kwamba "tutapigana dhidi ya masharti haya hatari kwa kila kitu tulicho nacho".
Changamoto hizi zinaweza kufikia Mahakama ya Juu ya Marekani ambayo, pamoja na wingi wa wahafidhina, inaweza kutoa uamuzi kumuunga mkono bwana Trump.
Magereza na mazingira kama vile makazi ya wahamiaji na waathiriwa wa ubakaji yatatengwa kulingana kuwa mwanamume au mwanamke chini ya mipango hiyo, ambayo wanaharakati wanasema itasaidia kuwalinda wanawake.
Lakini mashirika ya kutetea haki za watu waliobadili jinsia yanasema wanawake waliobadili jinsia wanaweza kuwekwa katika hatari kubwa ya unyanyasaji.
Nyaraka rasmi za utambulisho, ikiwa ni pamoja na pasi na viza, zingelazimika kueleza ikiwa mtu huyo alikuwa "mwanamume" au mwanamke." Raia wa Marekani hawataweza tena kuchagua "X" kama chaguo la tatu.
BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED