KILIO cha usimamizi usioridhisha wa Sera ya Maji ya Mwaka 2002, sasa una madai ya kuathiri upatikanaji wa majisafi kwa wakazi wa Kata ya Msowero, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.
Ni hali inayotajwa kuchochea ongezeko la magonjwa ya tumbo, kuhara na kipindupindu, huku ikiathiri uchumi katika sekta za kilimo na maisha ya kila siku ya wakazi wa eneo hilo.
Kukirejewa taarifa za Zahanati ya Msowero, idadi ya wagonjwa waliopata magonjwa ya tumbo imeongezeka kutoka 1,211 mwaka 2022/23 hadi 1,502 mwaka uliofuata 2023/24.
Wagonjwa hao wengi wanatajwa kutoka katika vijiji na shule za sekondari, katika Kitongoji cha A-Mzanini na Mzambarauni, ambavyo vyote havina huduma za maji safi.
Ofisa Tabibu wa zahanati hiyo, Ramadhani Mnyanga, anasema huwa wanapokea wagonjwa 27 wanaougua, shida zinazoambatana na tumbo kila wiki.
Ingawa inatajwa kuwapo juhudi za kuelimisha jamii juu ya usafi zinaendelea, bado kunalalamikiwa kuwapo mitazamo hasi kuhusu matumizi ya maji ya kuchemsha au yaliyotiwa dawa, hata kusababisha changamoto kubwa.
MAISHA KILA SIKU
Wakazi wa Msowero, kwa kawaida hulazimika kutembea umbali wa kilomita tano hadi sita, kutafuta maji kutoka kwenye bomba lililoko kijijini Msowero.
Hapo inatolewa ushuhuda wa Theresia Muga, mkazi wa Kitongoji A-Mzanini, anasema wanalazimika kutumia baiskeli kufuata maji.
Hapo anafafanua kwamba, ni jambo linalochukua saa tano hadi nane kila siku.
Vilevile, adha hiyo anaitaja inawalazimu kuchota na kutumia maji ya Mto Msowero na pengine ya visima, ambayo sio safi wala salama na kusababisha migogoro ya kifamilia na kuhatarisha usalama wa wanawake na watoto.
Jenipher Jackson, ni mkazi wa kijiji hicho anayeeleza kuwa, maji wanayotumia yanatoka kwenye visima visivyo salama, kutokana na kubaki wazi.
Poa anataja maji hayo yakachanganyika na taka mbalimbali kama nywele na kinyesi cha mifugo, hali inayowaweka kwenye hatari kubwa ya magonjwa.
“Maji tunayochota, kisima kipo wazi, hakina mfuniko. Wakati mwingi tunapata maji yenye mavumbi yenye uchafu wa mifugo na matambara machafu, licha ya kwamba hayakidhi mahitaji ya wakazi wote tuliopo hapa na hivyo kutuweka kwenye wakati mgumu kiafya,” analalamika Jenipher.
WAKWAMA KISERA
Diwani wa Kata ya Msowero, Eliud Malekela, anasema utekelezaji wa sera ya kisiasa ya maji inayogota mwaka huu, kwao imefika nusu safari, yaani asilimia 50 pekee.
Safari waendako, anajitetea kwamba wanajipanga na mamlaka ya kiserikali inayosimamia huduma za maji – RUWASA kufanikisha safari yao, akitaja maeneo makongwe yasyofikiwa na mradi huo: Majamba, Mkogwe na Kitongoji cha Mzambarauni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Msowero, Goodluck Magembe, anasema changamoto ya maji ilikuwa kubwa zaidi kati ya mwaka 2000 na 2019.
Anarejea kuwa, hali iliboreka kidogo kiasi, baada ya mradi binafsi uitwao Waridi ulipoanzisha vituo 26 vya kuhudumia maji.
Hata hivyo, anasema kiwango cha maji kilichoko, hakitoshelezi mahitaji ya wakazi, hivyo anaiomba serikali kuwasaidia mabomba ya visima vifupi 29.
Anafafanua kuwa, yakisambazwa kwenye maeneo yaliyokosa maji, yatasaidia kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji kulingana na mahitaji ya maji ya wakazi wa kijiji hicho.
Pia, anadokeza hatari inayowakabili iwapo jitihada zaidi hazitachukuliwa mapema kunusuru wakazi hao, kwamba wanaweza kuathirika kwa kupata magonjwa ya milipuko.
Anasema, maambukizi yakiwafikia itakuwa rahisi kwao kuambukizana, kutokana na mwingiliano walio nayo katika mahitaji na ununuzi wa vyakula, pia shughuli za kilimo cha mpunga na biashara ya mchele walio nayo.
Magembe anavitaja vijiji vinavyokabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji kuwa ni vitatu kati ya vinne vilivyopo kwenye Kata ya Msowero, vinajumuisha Mkogwe, Majambaa na Mambegwa, pia vitongoji kadhaa kutoka kwenye Kijiji cha Msowero.
RUWASA NA CHANGAMOTO
Kaimu Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kilosa, Mhandisi Silvia Ndimbo, anasema miradi ya maji inategemea malalamiko kutoka kwa jamii.
Anafafanua, licha ya kuwapo ufinyu wa bajeti isiyolingana na mahitaji, akigusia wanapatiwa bajeti ya shilingi bilioni 1.9 kwa mwaka wa fedha 2023/24 na bilioni 2.4 kwa mwaka 2024/25 zinazotumika kutoa huduma ya usambazaji maji wilayani humo.
Anasema, changamoto kubwa iliyopo katika maeneo mengi ni uharibifu wa vyanzo vya maji, kutokana na shughuli za kibinadamu.
NINI KIFANYIKE?
Hali ya ukosefu wa majisafi Msowero inafafanuliwa kuwa kielelezo cha changamoto kubwa katika utekelezaji wa Sera ya Maji ya Mwaka 2002.
Ili kufanikisha malengo ya sera hii, serikali inapaswa mambo kadhaa:
Mosi, ni kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya majisafi, hasa maeneo ya vijijini.
Pili, inatajwa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutumia majisafi na salama.
Tatu, inagusa haja ya kupanua ushirikiano na mashirika ya misaada ya kimataifa, katika kuongeza vituo vya maji.
Pia, kuna hoja inayoangukia serikali na wadau wengine wanapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wakazi wa Msowero wanapata huduma hiyo muhimu.
Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002, inaorodhesha malengo makuu matatu, inayoandaa mfumo unaokuza maendeleo bora, endelevu na sawa ya rasilimali za maji kwa manufaa ya Watanzania wote.
Pia, suala kuboresha afya na kupunguza umaskini wa wakazi vijijini, kwa kuboresha upatikanaji huduma za maji.
Ripoti za mwaka jana, za Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) zinaeleza kiasi kikubwa, kuwa mabilioni ya watu duniani wanaendelea kutaabika kutokana na kukosa huduma bora za maji na masuala ya usafi.
Hata hivyo ripoti hiyo inasema takribani watu bilioni 2.2 duniani kote, hawana huduma ya maji safi na salama ya kunywa.
Vilevile, kuna watu bilioni 4.2 hawana huduma salama za usafi na watu bilioni tatu wanakosa huduma za msingi kwenye sehemu za kunawa mikono.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED