WB yatakiwa kutoa kipaumbele Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:57 AM Apr 22 2024
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Natu Mwamba.
PICHA: MAKTABA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Natu Mwamba.

TANZANIA imeishauri Benki ya Dunia (WB) kuweka mbele vipaumbele vya maendeleo vya nchi za Afrika, ikiwamo kuzipatia fedha na ujuzi ili ziweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Natu Mwamba kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika la Benki ya Dunia) (WBG Africa Group 1 Constituency) uliofanyika Washington DC, nchini Marekani.

 Amesema WB imekuwa inasaidia kwa kiasi kikubwa nchi za Afrika na sasa wasaidie kuwekeza nguvu zaidi kwenye miradi ya maendeleo ili kuinua uchumi kwa haraka.

“Tunaiomba WB inapopitia matarajio yao iweke  kipaumbele kwa Afrika na kwa nchi moja moja na kutoa nyongeza ya rasilimali fedha,” amesema Dk. Mwamba.

Aidha, ameiomba benki hiyo kupeleka fedha zitakazoongezwa kupitia mzunguko mpya wa mfuko wa IDA 21 zipelekwe moja kwa moja kwa walengwa ili kupata matokeo chanya kwa haraka.

Aidha, ametoa wito kwa mashirika ya fedha ya kimataifa kutoa mikopo ya muda mrefu (Long Term Loans) isiyo na riba, ili nchi za Afrika ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo kikamilifu.

“Mikopo ya muda mfupi inaumiza nchi za Afrika, hivyo tunaomba mikopo iwe ya muda mrefu, miaka 50 hadi 70 na isiyo na riba,” amesisitiza Dk. Mwamba. 

Aidha, amekumbusha ombi la Serikali ya Tanzania katika mkutano wa 26 wa kundi la kwanza la nchi za Afrika uliofanyika Marrakech, Morocco mwaka jana, la kukifanya kiswahili kuwa miongoni wa lugha za mawasiliano wakati wa mikutano yake kutokana na kukua kwa lugha hiyo na kutumika kwenye mikutano mingine mingi ya Kikanda na Kimataifa.

“Kiswahili kimekuwa moja ya lugha inayotumika katika mikutano ya  Afrika Mashariki (EAC), SADC, AU na sasa inakwenda kupitishwa kutumika kwenye mikutano ya kimataifa,” amesema Dk. Mwamba.

Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi 22 wanachama ikiwa ni pamoja na Tanzania, Botswana, Burundi, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Gambia, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Ushelisheli, Sierra Leone, Somalia, Sudan, Sudan ya Kusini,Uganda, Zambia, na Zimbabwe.