Wawili jela miaka 20 kwa kukutwa na nyama ya twiga

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 09:38 AM May 10 2024
Twiga.
Picha: Maktaba
Twiga.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara imewahukumu watu wawili kwenda jela miaka 20 kila mmoja kwa kosa la uhujumu uchumi.

Wawili hao walikuwa wakituhumiwa kwa kukutwa na kichwa cha twiga, ngozi, pamoja na kilo 40 za mnyama huyo.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati, Victor Kimario, baada ya kusikiliza pande zote mbili.

Amewataja washtakiwa kuwa ni Paulo John (23) mkazi wa Kijiji cha Mapea na Athuman Misanya(31) mkazi wa Mamire.

Kimario alisema washtakiwa hao walitenda kosa hilo Februari 2, mwaka huu katika eneo la Hifadhi ya Burunge, ikiwa ni kinyume na Kifungu cha 86(2) (C) cha Sheria ya Wanyamapori, Sura 283 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi Kifungu cha 60(2) Sura 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Alisema washtakiwa wote walikuwa na vidhibiti hivyo wakiwa wamebeba kwenye ndoo.

Kimario alisema shahidi namba moja na namba mbili waliithibitishia Mahakama kuwa walikuwa wanne ila wengine walitoroka.

"Wote walikiri walikutwa porini kuchukua samaki japo wao wanadai ni samaki ila ilikuwa ni nyama ya twiga, hapana shaka kuwa ilikuwa nyama ya twiga," alisema Kimario.

Alisema upande wa mashtaka umethibitisha pasipo na shaka kuwa washtakiwa walikutwa na nyara za serikali licha ya wao kusema ni samaki.

Wakili wa serikali kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Getrude Kariongi, alisema hawana kumbukumbu za nyuma za watuhumiwa hao kufanya makosa ila kitendo cha kuua twiga ni kuharibu nembo ya Taifa.

Alisema kumtoa mnyama kwenye ikolojia ni kuathiri wanyama wengine wakati twiga ni kivutio cha watalii na aniingizia Taifa mapato.

Vile vile alisema nyama waliyokamatwa nayo ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani 20,000 (Sh.milioni 50).

Hivyo, aliiomba Mahakama hiyo kuitaifisha pikipiki waliyokutwa nayo na ndoo ili ziwe mali ya serikali.

Wakili wa utetezi, Festo Jackson alisema ni wateja wake ni mara ya kwanza wanatenda kosa kama hilo, umri wao ni nguvu kazi ya Taifa na wana wategemezi, hivyo aliiomba Mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Hakimu Kimario alisema nguvu walizokuwa nazo washtakiwa walizitumia vibaya kuihujumu serikali kwa kuua twiga ambaye ni nembo ya Taifa.