Watumishi Singida tangulizeni maslahi mbele ya wananchi- Waziri Silaa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 11:41 AM Oct 26 2024


WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa
Picha:Thobias Mwanakatwe
WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa

WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amewataka watumishi wa sekretarieti ya Mkoa wa Singida kutanguliza maslahi mbele ya wananchi katika utendaji wao wa kazi ili kuupaisha mkoa huo na taifa kimaendeleo.

Akizungumza na watumishi hao leo Oktoba 26, 2024 amesema iwapo watatanguliza maslahi ya wananchi kazi zitakwenda vizuri lakini wakitanguliza maslahi yao binafsi kazi hazitaenda vizuri jambo ambalo serikali haitegemei kuwa iwe hivyo.

"Tukiweka maslahi ya hapa Singida mbele kazi zitakwenda vizuri na tutaendelea kujenga taifa letu, niendelee kutoa wito tuchape kazi kwa kasi zaidi na pia tuyatangaze maendeleo makubwa yanayofanywa na serikali ili wananchi wayafahamu, "amesema Silaa.

Silaa amesema katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,imeleta fedha nyingi sana za kutekeleza miradi ya maendeleo  hivyo ni jukumu la watendaji kuhakikisha wanasimamia fedha hizo ili miradi iliyolengwa iweze kukamilika kwa wakati na ubora unaolingana na thamani ya fedha.