Watumishi Msalala wanaodaiwa kutesa wananchi wasimamishwa kazi

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 06:23 PM May 09 2024
MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita.
Picha: Maktaba
MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita.

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amelaani kitendo kilichofanywa na watumishi watano wa halmashauri ya Msalala kitengo cha ukusanyaji wa mapato ambao wameonekana kwenye kipande cha vitendo kilichosambaa kwenye mitandao ya kijamii kikionyesha wakitoa adhabu kwa wananchi wanaodaiwa kukwepa kulipa ushuru wa mazao.

Mhita akizungumza na vyombo vya habari kwa njia ya simu akiwa safarini amelisema, kitendo walichokifanya watumishi hao sio cha kiungwana nasio maelekezo ya serikali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kukusanya mapato kwani kinakiuka haki za binadamu.

Amesema, tukio hilo lilitokea Mei 02 Mwaka huu majira ya usiku katika viwanja vya makao makuu ya halmashauri ya Msalala kwa kuwapatia adhabu ya kuruka kichura chura, kugaragara, kuwabebesha mataili pamoja na kuwamwagia maji.

Aidha, amesema, baada ya serikali ya Wilaya kuiona video hiyo mtandaoni walilazimika kuchukua hatua ya kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria na Mei 07, waliachiwa kwa dhamana na sasa wamewasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuduma zinazo wakabili.

Mhita amesema, watumishi hao walipaswa kutoa elimu wakati walipowamakata wananchi hao nasio kujichukulia sheria mkononi na kuwapatia adhabu walizotoa, kazi zetu zinamiongozo, taratibu na kitendo hicho hakuna aliyefurahishwa nacho.

Hata hivyo amewataka watumishi wa halmashauri zote za Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama kufanyakazi kwa kuzingatia sheria nasio kujichukulia sheria mkononi na upelelezi unaofanywa na jeshi la polisi utakapokamilika watumishi wote watano watafikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo.