Watatu mbaroni mauaji ya mwanafunzi

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 08:25 AM Apr 22 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama.
PICHA: MAKTABA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama.

JESHI la polisi Mkoa wa Morogoro limewakamata watuhumiwa watatu kwa mauaji ya Makamu wa Rais wa Chuo cha St Joseph mjini Morogoro, Hajrath Mshamo (22), aliyekuwa akisoma mwaka wa tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema kwa kushirikiana na wananchi, wamekamata watuhumiwa watatu wakazi wa Morogoro.

Amewataja waliokamatwa kuwa ni Tyson Eliakim (20), Elias Lenjement (29) na Fredrick Nogwa (21) anayedaiwa kuwakodishia pikipiki watuhumiwa wenzake yenye namba za usajili MC.285 EDX.

Kamanda Mkama amesema vijana hao walipora simu ya mwanafunzi huyo kwa lengo la kujipatia kipato na katika harakati za kupambana kuokoa simu yake mmoja wao alimchoma kisu katika maeneo tofauti ya mwili wake na kusababisha kifo chake.  

Mwali wa mwanafunzi aliyeuawa kwa kuchomwa kisu Morogoro.
Kamanda amewataka wazazi na walezi kusimamia malezi pamoja na maadili ili vijana wajipatie kipato kwa njia ya halali na kupunguza uhalifu wa aina hiyo.

Tukio hilo lilitokea Aprili 16, mwaka huu, majira ya saa 2:30 usiku, wakati Hajrath na wenzake wakiwa kwenye hosteli za chuo hicho katika maeneo ya Mkundi, baada ya wanafunzi kumkamata kijana aliyekuwa amepakizwa kwenye pikipiki na mwenzake kukwapua simu ya mwanafunzi huyo.