WATU wanne wa familia moja wamelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro kutokana na kuungua moto baada mmoja wao kuwamiminia wenzake kimiminika kilichodhaniwa ni mafuta yenye asili ya mlipuko yaliyosababisha kuunguza nyumba yao iliyoezekwa kwa nyasi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Mei 19 mwaka huu saa mbili usiku katika Kijiji cha Gonja, Kata ya Pemba, wilayani Mvomero.
Mkama alisema kuwa kutokana na tukio hilo, polisi kwa kushirikiana na wadau wengine wa matukio ya moto wanafanya uchunguzi wa tukio hilo linalodaiwa kufanywa na Paschal Paul (18) na kusababisha majereha kwake pamoja na ndugu zake watatu.
Kamanda huyo alisema inadaiwa Paschal aliwakusanya ndugu zake watatu kwa lengo la kuwapasha habari, lakini akawamiminia kimiminika kilichodhaniwa kuwa ni mafuta yenye asili ya mlipuko.
Alisema kitendo hicho kilisababisha kuunguza moto nyumba yao iliyoezekwa kwa nyasi na kupata majeraha makubwa kwake pamoja na ndugu zake watatu na wote wamelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro.
Kamanda Mkama aliwataja majeruhi wengine wa moto ni Mathias Elias (34), mkulima; Augustino Elias ( 24), mkulima; na Anjela Elias (12), mwanafunzi na wote ni wakazi wa Kijiji cha Gonja, Kata ya Pemba, wilayani Mvomero.
Alisema inadhaniwa mtuhumiwa huyo ana changamoto ya afya ya akili kwa muda mrefu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED