MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa mwelekeo wa msimu wa mvua kwa miezi sita, zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi huu hadi Mei, mwakani.
Mwelekeo wa mvua za msimu ni katika maeneo ya magharibi mwa nchi, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini Magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini na maeneo ya kusini mwa Morogoro, ambayo yanapata msimu mmoja kwa mwaka unaoanza Novemba hadi kati ya Aprili na Mei, mwakani.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a, alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa mvua inatarajiwa katika kipindi cha nusu ya pili kuanzia Februari hadi Aprili, mwakani ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya Novemba, mwaka huu, hadi Januari.
Alisema mvua ya wastani hadi chini ya wastani inatarajiwa katika ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida, Dodoma, kaskazini na mashariki mwa mkoa wa Lindi na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa kuanzia Novemba hadi Aprili, 2025.
Pia alisema mvua ya wastani hadi juu ya wastani inatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, kusini magharibi mwa mkoa wa Lindi na kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.
Dk. Chang`a pia alisema mvua ya wastani hadi chini ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kanda ya Magharibi, Tabora, Katavi na Kigoma.
“Mvua imeshaanza tangu wiki ya nne ya Oktoba, mwaka huu, katika mkoa wa Kigoma na inatarajiwa kusambaa katika mikoa mingine kwenye wiki ya kwanza ya Novemba na kumalizika wiki ya kwanza ya Mei, mwaka kesho,” alisema.
Katika mikoa ya Kati ya Singida na Dodoma, alisema mvua katika maeneo hayo inatarajiwa kuwa ya wastani hadi chini ya wastani na inatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya Novemba na kwisha wiki ya nne ya Aprili na wiki ya kwanza ya Mei, mwaka kesho.
Kwa Nyanda za Juu Kusini Magharibi, alisema mvua ya wastani hadi juu ya wastani inatarajiwa katika mkoa wa Njombe, kusini mwa Mbeya, Iringa na Morogoro wakati zile za wastani hadi chini ya wastani, ikitarajiwa katika mikoa ya Rukwa na Songwe pamoja na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa katika wiki ya kwanza na ya pili ya Novemba na kuisha wiki ya kwanza ya Mei.
Dk. Chang`a alisema, katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na maeneo ya kusini na magharibi mwa Lindi, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani wakati katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Lindi na inatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.
Alisema mvua hiyo inatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Novemba kwa mikoa ya Lindi na Mtwara na wiki ya pili na ya tatu ya Desemba kwa Ruvuma huku ikitarajiwa kumalizika wiki ya kwanza ya Mei kwa mikoa ya Ruvuma na Mtwara na wiki ya nne ya Mei kwa Lindi.
“Izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vya mvua kubwa zaidi yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani. Mwelekeo wa mvua uliotolewa umezingatia mvua za msimu wa miezi sita na hali ya mvua katika maeneo makubwa.
“Kwa hiyo viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi vitazingatiwa katika utabiri wa kila siku na kila mwezi,” alisema Dk. Chang’a.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED