WATU mbalimbali wakiwamo wabunge wa Dar es Salaam na wakazi, wamemlilia aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk. Faustine Ndugulile, wakieleza kuwa alikuwa mtu mwenye upendo na mwenye kupenda ushirikiano.
Dk. Ndugulile aliyezaliwa Machi 31, 1969, alifariki dunia juzi akiwa nchini India alikokwenda kutibiwa na mwili wake unatarajiwa kuwasili leo mchana. Mwili wa Dk. Ndugulile, ambaye alikuwa Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, utazikwa katika makaburi ya Mwongozo, Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Msemaji wa familia ambaye ni mdogo wake, Wilbert Ndugulile, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba mwili wa Dk. Ndugulile, utawasili nchini leo saa 6:35 mchana.
Aidha, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge jana, mwili huo utapokewa na Naibu Spika, Mussa Azan Zungu, Katibu wa Bunge, wajumbe wa Tume ya Bunge, wawakilishi wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ratiba hiyo inaonesha kwamba mwili utapelekwa moja kwa moja Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo na kuhifadhiwa hadi Jumapili utakapopelekwa nyumbani kwake, Kigamboni.
Nyumbani kwa marehemu ambako ni takribani mita 200 kutoka kivuko cha Kigamboni, jana vilitawala huzuni na majonzi, huku wananchi na viongozi wa CCM, wabunge na watumishi wa manispaa ya Kigamboni, wakijumuika kuifariji familia.
Baadhi ya wananchi waliozungumza nyumbani kwa marehemu, walisema Dk. Ndugulile alikuwa mtu wa watu, akiwapigania wananchi wake na kutoa ushauri bila hila.
Walisema mbunge huyo alisimamia kile alichokiamini bila kuvunja sheria wala wakubwa zake.
Mbunge wa Mbagala (CCM), Abdallah Chaurembo, alisema Dk. Ndugulile alikuwa kiongozi aliyependa kushirikiana na alisikiliza ushauri wa watu wengine.
Alisema Dk. Ndugulile alikuwa mtu wa matokeo na alipenda kuona maendeleo yakifanyika na kuonekana.
Wabunge wengine waliofika nyumbani kwa marehemu ni mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abass, viongozi wa CCM mkoa na wilaya za Dar es Salaam.
Akizungumza na Nipashe jana, Meya wa Manispaa ya Kigamboni, Ernest Mafimbo, alisema kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, wananchi wa jimbo la Kigamboni wataaga mwili wa Dk. Ndugulile katika viwanja vya Machava keshokutwa.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan, Jumatatu ataongoza waombolezaji kuaga mwili wa Dk. Ndugulile katika viwanja vya Karimjee kwenye heshima za kiserikali ambazo zitahudhuriwa na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa likiwamo la Afya Duniani (WHO), wabunge na mawaziri.
Wilbert ambaye ni msemaji wa familia kuhusu msiba huo, alisema jana kwamba baada ya mwili kuwasili na kupelekwa Lugalo, familia, ndugu jamaa na rafiki, wataendelea na maombolezo nyumbani kwake, Kigamboni.
“Baada ya mwili kuwasili na kupelekwa Lugalo, familia tutaendelea na maombolezo hadi tarehe 2 Desemba. Mwili utatolewa Lugalo na kupelekwa Parokia ya Mtakatifu Imaculata Upanga kwa ajili ya ibada. Baada ya hapo mwili utapelekwa Karimjee kwenye mazishi ya kitaifa,” alisema.
Alisema baada ya Karimjee, mwili utalala nyumbani kwake Kigamboni na Jumenne, mwili utapelekwa viwanja vya Machava kwa ajili ya wananchi kumuaga.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED