HUKUMU ya Kesi ya Jinai namba 1883/2024 inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk.Yahaya Nawanda inatarajiwa kusomwa leo Novemba 29,2024 katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Mwanza.
Dk.Nawanda alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Julai 9,2024 na kusomewa shtaka moja la kulawiti kinyume na kifungu namba 154 (1) (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16.
Ni baada ya danadana za muda mrefu zilizokuwa zikifanywa na mawakili upande wa Jamhuri dhidi ya waandishi wa habari zikilenga kuukosesha umma haki ya kupata taarifa juu ya mwenendo wa shauri hilo.
Licha ya shauri hilo la ulawiti kutakiwa kusikilizwa nyuma ya kamera (faragha), kwa mujibu wa kifungu cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 Kifungu namba 186(3).
Lakini kwa mujibu wa Sheria za Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 20 kifungu namba 186, shauri hilo lilitakiwa kuwa wazi kutokana na kuwa na maslahi kwa umma.
Hivyo ili kulinda utu wa mtendewa (binti) Hakimu Mfawidhi Mkuu wa Mahakama hiyo Erick Marley aliruhusu waandishi kupewa taarifa za mwenendo wa shauri hilo kila baada ya kipindi cha usikilizaji shauri kuisha bila wao kuingia mahakamani moja kwa moja.
Licha ya Hakimu Marley kutoa ruhusa hiyo bado mawakili hawakutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari hivyo kila shauri lilipokuwa likiisha hawakujulikana walikopitia hivyo kesi hiyo kushindikana kuripotiwa.
Dk.Nawanda anadaiwa kutenda kosa hilo Juni, 2, 2024 la kumwingilia kinyume na maumbile (kumlawiti) Mwanafunzi wa Chuo kimoja mkoani Mwanza kosa analodaiwa kulitenda katika eneo la maegesho ya magari, lililoko Rock City Mall wilayani Ilemela mkoani hapa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED