Barrick yapokea kwa furaha maamuzi ya mahakamu ya juu

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 02:59 PM Nov 29 2024

Mahakama ya Ontario yatupilia mbali shauri kuhusu Mgodi wa North Mara
Picha:Mtandao
Mahakama ya Ontario yatupilia mbali shauri kuhusu Mgodi wa North Mara

KAMPUNI ya kuchimba Dhahabu ya Barrick imepokea kwa furaha uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Ontario ya Nchini Canada ya kutupilia mbali madai yaliyotolewa na baadhi ya wakazi Mkoa wa Mara waliokuwa wakilalamikia ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Askari wa Jeshi la Polisi Tanzania jirani na mgodi wa dhahabu wa kampuni hiyo wa North Mara.

Mahakama hiyo iliamua kwamba Ontario haikuwa jukwaa mwafaka la kusikiliza madai hayo.

Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, amesema kampuni hiyo imekanusha mara kwa mara kile inachokiona kama madai yasiyo na msingi yanayotolewa na asasi chache zisizo za serikali zenye mrengo wa kiuanaharakati zinaodai kuwapo kwa ukiukwaji wa kihistoria wa haki za binadamu katika maeneo  yanayozunguka mgodi wake wa North Mara.

“Tunajivunia mafanikio tuliyoyapata  nchini Tanzania kutokana na ushirikiano wetu na  Serikali ya nchi hiyo kupitia ubia wa Twiga. Mchango wa mapato ya migodi yetu umeleta mageuzi katika uchumi wa nchi hiyo wakati uwekezaji wetu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya jamii za wenyeji, ukiambatana na mkakati wetu wa kuleta maendeleo ya jumla, umeboresha hali ya maisha yao," amesema.