Tanzania, China zashirikiana kuimarisha masomo ya Sayansi

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:38 PM Jul 11 2024
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba kushoto na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal University (ZJNU) cha China Prof. Huang Xiao kulia, wakisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano.
Picha: Maulid Mmbaga.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba kushoto na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal University (ZJNU) cha China Prof. Huang Xiao kulia, wakisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano.

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal University (ZJNU) cha nchini China kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba, amesema ushirikianao huo utasaidia kuanzisha kituo cha Elimu ya Sayansi na Kidijitali na kuifanya TET kuwa kituo cha mafunzo cha kikanda katika masomo ya sayansi.
 
Pia amebainisha shughuli mbalimbali zitakazotekelezwa kutokana na mkataba huo ikiwemo kuimarisha uwezo wa wakuza mitaala, walimu mahiri na wakufunzi wa masomo ya sayansi kupitia kozi fupi.
 
“Kuimarisha uwezo wa wakuza mitaala kupitia kozi za muda mrefu kupitia fursa za mafunzo ya shahada ya uzamili na uzamivu. Kufanya shughuli za kubadilishana maarifa kwa kufanya tafiti.
 
“Kushirikiana katika kuandaa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kama vile vitabu vya kiada, miongozo, moduli na matini zenye maudhui ya kieletroniki,” amesema Dk. Aneth.

Ameongeza kuwa kutakuwa na ziara za kimasomo za kubadilishana wataaluma kutoka TET na ZJNU ili kupeana uzoefu na ujuzi kwenye maeneo mbalimbali ya kielimu hasa elimu ya sayansi na kidijitali.
 
Eneo lingine ni kuweko kwa ziara za wanafunzi, wanaotaka kufanya programu fupi na kushirikiana katika kuandaa mikutano na makongamno ya kielimu ya kimataifa itakayofanyika nchini China au Tanzania kila mwaka. 
 

1

Mkuu wa Chuo cha ZJNU, Prof. Huang Xiao, amesema ushirikiano huo unasisitiza dhamira yao ya pamoja ya kuendeleza elimu na kukuza uvumbuzi kuhusu elimu ya kidijitali. Na kwamba wana historia yenye manufaa ya ushirikiano na taasisi za elimu Afrika.
 
Amesema katika chuo hicho wamekuwa wakitekeleza mkakati wa utandawazi na kuanzisha mawasiliano ya kina na vyuo vikuu kote ulimwenguni, kama Chuo Kikuu cha Kansas nchini Marekani na cha Malkia Uingereza.
 
“Leo, tunarasimisha ushirikiano wetu na TET kwa kutia saini mkataba wa makubaliano, unaozingatia maeneo mawili muhimu elimu ya STEM na ya kidijitali, lakini pia katika maeneo mengine kama vile kubadilishana, uwezo wa utafiti,” amesema Prof Huang.
 
Amesema ushirikiano huo pia utaboresha matokeo ya elimu na kuwatayarisha wanafunzi kwa siku zijazo. Na kwamba inaonyesha imani yao katika kuleta mabadiliko ya elimu na azimio la kutoa fursa ambazo ni jumuishi, zinazolingana na zinazotazamia mbele.
 
“Kwa pamoja, tunaanza safari ambayo inaahidi sio tu kuimarisha maisha ya wanafunzi wetu lakini pia kuchangia ipasavyo katika nyanja pana ya elimu katika nchi zetu zote mbili.
 
“Kwa utekelezwaji wa mtaala mpya, nina imani kuwa juhudi zetu za pamoja zitaleta matokeo ya ajabu, na kutengeneza njia kwa mustakabali mzuri na wa ubunifu zaidi,” amesema Prof. Huang.