SERIKALI imetangaza kuwa Novemba 27 mwaka huu ni siku rasmi ambayo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika.
Vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu nchini vilihudhuria tukio hilo la kutangazwa tarehe ya uchaguzi huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakikupeleka mwakilishi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa, alitangaza tarehe rasmi ya uchaguzi huo jana jijini hapa mbele ya viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa na wadau wengine wa maendeleo.
"Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019, ibara 4 (1-3) (Matangazo ya Serikali Na. 571, 572, 573 na 574) ya mwaka 2024, ninautangazia umma wa watanzania na vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu kuwa tarehe 27 Novemba 2024 itakuwa ni siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara.
"Upigaji wa kura utaanza saa 12:00 asubuhi na kumalizika saa 10:00 jioni," alisema Mchengerwa na kueleza kuwa nafasi zitakazogombewa ni mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji (kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake), wajumbe wa halmashauri ya kijiji (kundi la wanawake) na wenyeviti wa vitongoji katika mamlaka za wilaya.
"Kwa nafasi hizo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za wilaya za mwaka 2024," alisema.
Waziri huyo alisema uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo za mwaka 2024.
"Kwa mujibu wa kanuni hizi, ili kuwafahamisha wananchi majina ya maeneo na mipaka ambayo itahusika katika kujiandikisha na upigaji kura, wasimamizi wa uchaguzi watatangaza majina na mipaka ya vitongoji vilivyoko katika eneo la halmashauri husika siku 72 kabla ya siku ya uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji, mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa mtaa, wajumbe wa serikali ya kijiji na wajumbe wa kamati ya mtaa," alisema.
Waziri huyo alisema uteuzi wa waandikishaji na waandaaji orodha ya wapigakura kwa mujibu wa kanuni hizo, utafanywa na msimamizi wa uchaguzi atakayeteua watumishi wa umma watakaoandikisha na kuandaa orodha ya wapigakura siku 52 kabla ya siku ya uchaguzi.
"Uandikishaji wapigakura kwa mujibu wa kanuni hizi, uandikishaji na uandaaji wa orodha ya wapigakura utaanza siku ya 47 kabla ya siku ya uchaguzi na utafanyika kwa muda wa siku 10," alisema.
"Muda wa kuchukua na kurudisha fomu za uteuzi kwa mujibu wa kanuni hizi, mtu yeyote anayekusudia kugombea nafasi za uongozi, atatakiwa kuchukua fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi husika siku zisizopungua 26 kabla ya siku ya uchaguzi kwa kadri itakavyoelekezwa na msimamizi wa uchaguzi na kutakiwa kurejesha fomu husika ndani ya muda wa siku saba tangu siku ya kwanza ya uchukuaji fomu iliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi," alisema.
Waziri huyo alisema wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi watatakiwa kuwa wanachama na wadhamininiwa wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje CHADEMA, John Mrema, alipotafutwa na Nipashe jana, alisema walishindwa kushiriki tukio hilo kutokana na viongozi wakuu kuwa wagonjwa baada ya kutoka mahabusu walikoshikiliwa na polisi.
"Msajili wa Vyama vya Siasa aliandika barua ya mwaliko kwa mwenyekiti wa chama Agosti 13 mwaka huu na siku hiyo ndiyo mwenyekiti alikuwa mahabusu pamoja na makamu wake na katibu mkuu, hivyo mwaliko haukuwafikia, lakini pia walipotoka walikuwa wagonjwa kwani walikuwa wameumizwa na polisi walipokuwa mahabusu," alisema Mrema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED