SIKU YA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU DUNIANI; JKCI kutoa huduma bure

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 12:49 PM May 10 2024
Nesi akimfanyia vipimo mgongwa wa Shinikizo la Damu.
Picha: Maktaba
Nesi akimfanyia vipimo mgongwa wa Shinikizo la Damu.

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), inatarajia kuadhimisha Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani, kwa kutoa huduma bure kwa wananchi, kwa kuwapima na kuwapa matibabu, kwa siku mbili.

Kila mwaka siku hiyo huadhimishwa Mei 17, huku JKCI ikiiadhimisha kwa kutoa huduma katika tawi lake, JKCI-Dar Group jirani na TAZARA, Wilaya ya Temeke,  mkoani Dar es Salaam.

Utoaji huduma hizo ni mpango endelevu wa tiba mkoba ujulikanao  'Samia Suluhu Hassan Outreach Services' kwa kufanya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi mikoa tofauti.

Upimaji huo, utafanyika bila malipo yoyote, kwa watoto na watu wazima kuanzia Mei 16 hadi 17, mwaka huu, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10.

Aidha katika kambi hiyo, kutakuwa na wataalamu wa lishe watakaotoa elimu ya lishe bora itakayowapa wananchi uelewa na kufuata mtindo bora wa maisha na kuepukana na NCDs.

Imesema taarifa hiyo leo, iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano JKCI, Anna Nkinda.