Sheria ya ukatili kufumuliwa

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:25 AM Apr 19 2024
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Tunza Malapo.
PICHA: MAKTABA
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Tunza Malapo.

SERIKALI imesema ipo tayari kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na vitendo vya ukatili, ukiwamo wa kijinsia, ambavyo vimeendelea kukithiri nchini ili wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria na hatimaye kuvikomesha.

Akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa wabunge, amesema serikali inatambua kukithiri kwa vitendo hivyo, hususani ukatili wa kijinsia, katika baadhi ya maeneo nchini na kwamba suala hilo liko chini ya wizara mbalimbali na hatua zimekuwa zikiendelea kuchukuliwa.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Tunza Malapo, aliyetaka kujua mkakati wa serikali kudhibiti vitendo hivyo, amesema : “Kwa kuwa nimekiri kwamba tatizo hili lipo kwa baadhi ya maeneo nchini na hatua kali zinachukuliwa, lakini yanajirudia kutokana na sheria zake kuwa si kali sana, jambo hili ni mtambuka na linagusa wizara nyingi na kila wizara inaweka sheria yake katika kukinga jambo hili.

“Kwahiyo tunapokea ushauri wa kufanya mapitio kwa sheria hizi malengo yetu yakiwa  kuhakikisha jamii inakuwa salama na wale wote wanaoendelea kufanya matendo haya wanachukuliwa sheria kali. Tunatamani tuone jambo hili likikoma kwenye jamii.”

Aidha, Waziri Mkuu ameitaka jamii kuzingatia mila na na desturi njema ili kuepuka kutumbukia katika matendo kama hayo ya kikatili kwa kuwa kila mmoja ana haki ya kuishi.

“Kwanza tupunguze ulevi holela unaosababisha watu kutenda mambo kinyume cha akili zao, imani na mila potofu pamoja na malezi ambavyo vimekuwa chanzo cha matukio hayo. Pale panapohitajika mabadiliko ya sheria na kanuni, tuko tayari kuileta hapa bungeni ili kuzibana zaidi,” amesisitiza.

Awali, Malapo amesema matukio ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, wanawake, makundi mengine pamoja na wanyama, yamekithiri nchini licha ya adhabu mbalimbali kutolewa, hivyo kuitaka serikali kuweka muswada mezani kwa ajili ya kuongeza au kubadili adhabu zinazotolewa ili zikidhi haja ya kukomesha matukio hayo.

LESENI ZA MADINI 

Waziri Mkuu amesema serikali ina nia ya kuyatwaa maeneo yote makubwa ya madini yanayomilikiwa na wawekezaji, bila kufanya kazi yoyote na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo ili kuwasaidia kupata fursa ya kuchimba madini.

Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kishapu (CCM) Boniface Butondo, aliyetaka kupata ufafanuzi kuhusu kauli ya serikali kudhibiti ongezeko la leseni zinazohodhi maeneo makubwa bila kufanyiwa kazi na kuwanyima fursa wachimbaji wadogo wanaohitaji maeneo hayo. 

 “Wako wanaomiliki maeneo makubwa ya madini lakini hakuna kazi yoyote inayofanyika kwenye maeneo hayo na wengine hawajalipia gharama za kutenda na kutekeleza shughuli hizo. Lakini  waziri alishatoa maelekezo hapa kwa wakuu wa mikoa kufanya mapitio na kutwaa maeneo hayo,” amesema Majaliwa.

Pia amewaagiza makamishna wa madini na mameneja wa mikoa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati ili serikali ifute leseni hizo na kuanza kuyagawa kwa wachimbaji wadogo.

MICHANGO YA MAAFA

Katika hatua  nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya ambao pia ni wenyeviti wa kamati za maafa katika maeneo husika kutekeleza wajibu wao wa kutoa mrejesho wa michango na misaada inayotolewa na wadau mbalimbali katika kukabiliana na maafa yanayotokea.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuweka uwazi na imani kwa jamii na wadau ili waendelee kuhamasika kutoa michango zaidi, ili kuzisaidia jamii zinazopatwa na maafa pamoja na urejeshaji wa miundombinu.