Serikali yasikia kilio wanandoa kutenganishwa mikoa ya kazi

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 03:32 PM Apr 22 2024
Wanandoa kutenganishwa mikoa ya kazi.
PICHA: MAKTABA
Wanandoa kutenganishwa mikoa ya kazi.

SERIKALI imesia kilio cha wabunge cha kutaka watumishi wa serikali walio katika ndoa kutotenganishwa na wenza wao sehemu wanapofanya kazi, ikisema mwaka huu wa fedha watahakikisha wenza wanapohamishwa wanakwenda na wenza wao.

Akizungumza bungeni  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema suala hilo litazingatiwa kwenye msawazo wa watumishi wa umma ambao wataufanya mwaka huu ikiwa ni hatua ya kukabiliana na upungufu wa watumishi.

“Kila mtumishi mwenye mwenza wa kweli atakwenda kufanya kazi mahali pamoja, siyo lazima kiwe kituo kimoja cha kazi kama ni walimu basi mmoja atafundisha shule hii na mwingine atafundisha shule hii. Lakini mahali ambapo jioni wanakwenda kulala pamoja.”

“Ukiwa na cheti cha ndoa na umefunga ndoa ya kweli maana kuna ndoa nyingine za uongo uongo, hili hatuwezi kulikubali, tutahakikisha mwanya huu wa msawazo basi kila mtumishi tunawaunganisha ili waweze kufanya kazi kwa raha na starehe,” amesema.

Amebainisha jambo hilo limekuwa likiwakera na wabunge wengi wamekuwa wakipeleka maombi katika ofisi yake na hatua hiyo itaongeza tija katika utendaji wa kazi.

Simbachawene amesema tatizo la upungufu wa watumishi katika baadhi ya maeneo inachangiwa na watumishi kurundikana katika baadhi ya maeneo.

Amesema: “Wabunge msirudi tena kulalamika kwa sababu tutakapoanza operesheni haitamwacha mtu na haitakuwa na upendeleo lakini tutazingatia hali na sababu mahususi waliyonayo watumishi”.