Serikali yakemea wanaotoza ushuru wateja wadogo

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:24 AM May 10 2024
Ushuru kwa wateja wadogo wakemewa.
Picha: Maktaba
Ushuru kwa wateja wadogo wakemewa.

SERIKALI imekemea vikali tabia ya baadhi ya wasimamizi wa mialo ya samaki kuwatoza ushuru wateja wanaonunua chini ya kilo 30 kwa matumizi ya nyumbani na kuziagiza halmashauri kukomesha jambo hilo kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti, ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira, aliyehoji serikali ina mikakati  gani wa kupunguza na kufuta baadhi tozo ili kuleta unafuu kwa walimu. 

Amesema sheria inaelekeza wafanyabiashara wa samaki kutozwa ushuru hata wakinunua chini ya kilo 30, lakini wateja wa kawaida wanaonunua kwa matumizi ya nyumbani hawapaswi kutozwa isipokuwa wakinunua zaidi ya hapo.

Mnyeti amesema mwaka 2020 na 2022 serikali ilifanya maboresho ya tozo mbalimbali, ikiwamo baadhi ya leseni kuunganishwa na tozo zingine kupunguzwa na wizara itaendelea kuboresha na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi kadiri itakavyowezekana na kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi nchini.

“Tozo ambazo zilipunguzwa ni ushuru wa dagaa wanaozalishwa Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Bahari ya Hindi kutoka Dola 0.16 (Sh. 412.6) hadi Dola 0.1 (Sh.257.9) kwa kilo na tozo ya dagaa wa Ziwa Tanganyika kutoka Dola 0.5 (Sh. 1,289.33) hadi Dola 0.3 (773.6) kwa kilo,” amesema.

Ametaja tozo zingine zilizobadilishwa kuwa ni za kusafirisha minofu ya sangara nje ya nchi iliyopunguzwa kutoka Dola 0.2 (Sh. 515.7) hadi Dola 0.1 (Sh. 257.9) kwa kilo.

Pia amesema serikali imepunguza ushuru wa uingizaji mazao ya bahari kutoka Dola 2.5 (Sh.6,446.6) hadi Dola 0.5 (Sh.1289) kwa kilo kwa ngisi, pweza na kaa na  gharama ya ada za leseni za kusafirisha dagaa kutoka Dola 1,000 (Sh. 2,578,650) hadi Dola 250 (Sh. 644,663) kwa dagaa wa maji chumvi na maji baridi.