Samia ajivunia ongezeko la biashara Tanzania, Uturuki

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:58 AM Apr 19 2024
RAIS Samia Suluhu Hassan.
PICHA: IKULU
RAIS Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Uturuki, zimeshuhudia ongezeko la biashara kwa kipindi cha miaka 10 kutoka dola za Marekani milioni 60 mwaka 2011/2012 hadi dola za Marekani milioni 300 mwaka 2022/2023.

Amesema hayo nchini Uturuki wakati akihutubia wageni mbalimbali baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ankara, nchini humo.

“Kama mwanachama wa G20, tunatarajia msaada wa Uturuki katika changamoto mbalimbali zinazoikabili Afrika yakiwamo madeni, mageuzi ya usanifu wa fedha duniani na kuhakikisha fedha za maendeleo endelevu ili kukabiliana na mapambano ya kuleta haki na usawa.

“Tumeendelea kuvutia washirika wanaoheshimika kufanya miradi ya kuleta mageuzi ya miundombinu nchini Tanzania, tunayo kampuni Yapi Merkezi kutoka katika nchi hii ya Uturuki, ambayo inashirikiana nasi katika kufanikisha mradi wetu wa treni ya kisasa (SGR),” amesema.

Rais Samia amesema hadi Desemba, mwaka jana,  ilisajiliwa miradi mipya 526 mikubwa ya uwekezaji yenye thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 5.6, ambayo ni ongezeko la asilimia 58.

Kuhusu shahada aliyotunukiwa na kukabidhiwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ankara,   Prof. Necdet Unuvat, kwenye hafla iliyofanyika chuoni hapo, Rais Samia amesema amepokea kwa niaba ya wachapakazi wote wa kike na wa kiume wa Tanzania.

“Ninapokea heshima hii kwa niaba ya wanaume na wanawake wachapakazi nchini Tanzania. Mimi ni kiongozi wao tu, na ninafanya yote ninayofanya kwa niaba yao. Ninapotafakari nyuma na kukumbuka changamoto na bidii ya watu wangu, ninajisikia unyenyekevu sana kukubali shahada hii ya heshima ya udaktari.

“Natoa shukrani zangu kwa Seneti ya Chuo Kikuu cha Ankara kwa uamuzi wao wa kunipatia Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Uchumi. Ninanyenyekea na kuheshimu kutambuliwa katika elimu hii ya kifahari ya chuo kikuu ambayo kimataifa inawekwa katika daraja la juu,” amesema. 

Rais Samia pamoja na viongozi wengine, waliwasili juzi nchini Uturuki kwa ziara ya kikazi.