Sababu idadi ndogo matibabu watoto wenye kifafa zaanikwa

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:01 AM May 10 2024
Idadi watoto wenye kifafa yapungua.
Picha: Maktaba
Idadi watoto wenye kifafa yapungua.

TAASISI ya Wazazi wa Watoto Wanaoishi na Kifafa, imezindua kampeni ya kuhamasisha jamii kuhusu uelewa wa maradhi hayo na kueleza kuwa, idadi kubwa ya waliokuwa wakihudhuria kliniki imepungua kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo suala la bima.

Daktari Bingwa Mbobezi wa Afya na Magonjwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Said Kuganda, ambaye ni Mwenyekiti wa taasisi hiyo ambayo pia, inalenga wanaoishi na hali ya kifafa, ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo hospitalini hapo.

Bingwa huyo amesema: “Zamani tulikuwa na mfuko wetu maalum tunatafuta wafadhili wanatuongezea fedha kisha tunatafuta dawa kiasi, hivyo aliyekuwa akikwama tulikuwa tunampatia dawa.

“Ilipokuja bima ya afya, watoto wengi walijiunga huko. Kwa hiyo dawa za kawaida zikawa zinapatikana huko. Kasi ya mfuko wetu ikapungua kwa kuwa, wengi walijiunga katika bima ya afya, wakawa wanapata huduma hata kwa watu wazima.

“Bahati mbaya bima ya watoto ikafutwa ili kuanzisha iliyo bora zaidi. Tangu ifutwe na inayoboreshwa bado haijaja, tumerudi kwenye changamoto, wazazi wengi wanalalamika, hawaji tena kwenye kliniki kwa kuwa, kila wakija wanaambiwa wanunue dawa, bima haifanyi kazi tena.

“Tumebaki na hii changamoto ambayo kidogo tunasema tuongeze sauti ifike kwa jamii kujaribu kuangalia namna wanavyoweza kusaidia jambo hili.

“Tunajua serikali inafanya vizuri, lakini kama wananchi tufanye juhudi kujulisha serikali kwamba, kuna watu wenye hizi hali hawana bima, hivyo imekuwa shida na wanapungua katika kliniki zetu.”

Amesema mtazamo wao bado anaitegemea serikali na wanaamini wataboresha huduma ikiwamo wenye kifafa.

“Tunaamini kitakachokuja kitakuwa kizuri zaidi, lakini tunataka serikali ijue kuna watu wanashindwa kuja kupata huduma kwa sababu ya hizi changamoto,” amesema.

Hata hivyo, mtaalum huyo ameishukuru serikali kwa kuwa kwa mwaka huu, baadhi ya dawa nzuri mpya zimeanza kuingizwa katika kifurushi cha bima, lakini changamoto iliyoko ni watu hawana kifurushi chenyewe.

“Watoto wengi wanachukua bima shuleni, kwa hiyo kwa watoto wa kifafa wanaougua sana huwa hawaendi shuleni. Na asipokwenda anajikuta hapati huduma. Tunaposema kuondoa unyanyapaa ni kujaribu kusaidia katika haki zao za msingi,” amesema.

Amesema wanaomba serikali iangalie kwa kuwa wazazi wameshachoka na watoto wao wanahitaji tiba.

“Wengi wamepungua na hatuwezi kusema kwa namba. Sababu zipo nyingi hii ni kutokana na swali, lakini nyingine ni unyanyapaa ambao kabla hawajapata tiba nzuri unakuta mganga wa kienyeji ameshamwambia  (mzazi au mlezi) tiba iko huku.

“Kwa sasa ukitembelea Ifakara, mkoani Morogoro kwa sababu ya visababishi vipo vingi imegundulika watu wengi pale wameathirika tatizo la kifafa, wapo kwenye matibabu na utafiti unaendelea, lakini inaonyesha kuna utofauti na maeneo mengine.

“Ila kila maeneo Tanzania kuna watu wanaishi na hali ya kifafa. Mfano hapa (Tanzania) wanasema karibu katika watu 1,000  kati ya 20 mpaka 37 huwa na hiyo hali, lakini kwenye hayo maeneo ambayo hali hii inaonekana ni kubwa zaidi,” amesema.

Amesema wamekuwa wakihamasisha wenye kifafa kuwa makini na kufuatilia dawa na matibabu kwa ujumla kwa kuwa, tiba sahihi ikifuatiliwa mara nyingi matukio kama hayo hupungua.

Kuhusu kampeni waliyozindua, mtalaam huyo amesema, itafanyika kwa mwaka mzima na ifikapo mwezi Novemba, mwaka huu, watakuwa na mdahalo wa kitaifa kuhusu kifafa na namna bora ya kuwasaidia wanaoishi na hali ya kifafa.

Mgonjwa anayeishi na kifafa, Dk. Mary Kipingili, amesema kaulimbiu ya kampeni hiyo inasema, “Elimika juu ya kifafa, tokomeza unyanyapaa, pata tiba sahihi.”

Ameishukuru serikali kwa kutoa kipaumbele na kuboresha afya za wananchi wake, hasa katika kuzuia na kutibu magonjwa yasiyoambukizwa, kifafa kikiwa ni miongoni mwa maradhi hayo yanayotokana na hitilafu katika mfumo wa umeme wa ubongo.

Amesema kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani watu milioni 50 wanasumbuliwa na hali za kifafa, huku  katika Bara la Afrika kukiwa na zaidi ya watu milioni 10 wanaishi na hali hiyo.

“Inakadiriwa kuwa watu milioni sita hubainika na hali hii kila mwaka.  Hapa Tanzania zaidi ya watu milioni moja huishi na hali za kifafa.

“Kwa bahati mbaya kabisa uelewa wa wanajamii kuhusu hali hizi za kifafa bado ni mdogo, hivyo kumekuwapo na vitendo vya unyanyapaa na kubaguliwa kwa watu wanaoishi na hali za kifafa,” amesema.

Mary amesema unyanyapaa na kubaguliwa imechangia wao kukosa haki zao za msingi katika maisha yao ya kila siku na hivyo kudhoofisha ubora wa maisha yao. “Kumekuwa na visa mbalimbali vya kufukuzwa shule au kutopelekwa shule kabisa, kutoajiriwa au kufukuzwa kazi, kuvunjika kwa mahusiano au ndoa unapogundulika kuwa na hali za kifafa, na hata kufanyiwa vitendo vya kikatili vinavyotokana na imani za kishirikina,” alibainisha.

Aidha, amesema  vitendo hivyo huleta msongo wa mawazo na kwamba, inaripotiwa kuwa takriban watu watano kati ya 10 wanaoishi na hali za kifafa wanapata maradhi ya wasiwasi au sonona na huwa katika hatari ya kufariki mapema mara tatu zaidi ya watu wa kawaida.

Amesema wengi wanaoishi na hali hizo wamekuwa hawaendi katika vituo vya afya kupata tiba sahihi, hivyo kuchangia usugu au ukali wa tatizo pamoja na madhara mengine.

“Tunaungana na serikali pamoja na taasisi zote za kijamii na za kitaaluma katika jitihada zao na kampeni za  kuelimisha jamii kupata ufahamu sahihi kuhusu kifafa ili  kutokomeza unyanyapaa,” amesema.