RC Kunenge awapokea Madaktari Bingwa wa Mama Samia

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 03:25 PM Jun 03 2024
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.
Picha: Julieth Mkireri
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amepokea Madaktari Bingwa wa Mama Samia 45 ambao watatoa huduma za kibingwa katika Halmashauri tisa za mkoa huo.

Madaktari hao kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini wanatarajiwa kufanya kazi kwa siku tano kwa Mkoa huo na baada ya hapo wataendelea katika mikoa mingine kutoa huduma kama hizo.

Akizungumza baada ya kukutana na Madaktari hao Juni 3, 2024 Mjini Kibaha, Kunenge amemsukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kampeni hiyo aliyoianzisha ambayo itawasaidia wananchi wengi wenye uhitaji wa huduma za kibingwa.

Kunenge amesema wapo wananchi ambao wanashida na hawana uwezo wa kuwafikia madaktari hao, hivyo alichokifanya Rais kusogeza huduma hiyo itawasaidia walio wengi kutumia fursa hiyo ya kupata matibabu kwenye Hospitali zilizopo katika Halmashauri zao.

"Madaktari ni kazi ya wito na hiki mnachokofanya ni kama mnajitolea, wakati mnatoa huduma hizi muwajengee uwezo Madaktari wetu Ili mnapoondoka waendeleze huduma hizi," amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akiwa katika picha ya pamoja na madaktari Bingwa wa Mama Samia.


Afisa kutoka Wizara ya Afya John Meena amesema kampeni hiyo imeanza katika mikoa mwingine kwa Madaktari bingwa kutoka Hospitali mbalimbali na wakimaliza Mkoa wa Pwani wataendelea maeneo mengine kuwafikia wananchi wenye uhitaji.

Meena amesema timu ya afya ya Mkoa wa Pwani watapata fursa ya kujiongezea uwezo wa huduma za kibingwa kutoka kwa Madaktari hao na kwamba Madaktari hao 45 wamegawanywa katika Hospitali za Halmashauri tisa za mkoa huo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dk.Benedicto Ngaiza amewataka wananchi wenye uhitaji wa huduma za kibingwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo.

Mkoa wa Pwani una Hospitali 13 , vituo vya afya 50, Zahanati 388 pamoja na kliniki za kujifungulia 22.