RAIS Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kutokana na kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali David Msuguri (104), aliyefariki dunia jana katika Hospitali ya Rufani ya Bugando, Mwanza wakati akipatiwa matibabu.
Rais Samia alituma salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, huku akimwelezea kuwa kiongozi aliyetimiza wajibu wake kwa miaka 46 kwa kujitoa kwa nchini yake.
"Kwaheri Jenerali, ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda, makamanda, wapiganaji wastaafu, wapiganaji walio katika utumishi, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa kuondokewa na shujaa wetu, mpendwa wetu, mwalimu, mshauri na kiongozi wetu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali (Mstaafu) David Bugozi Musuguri," aliandika katika WhatsApp Channel yake.
"Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha yake ya miaka 104, ambapo miaka 46 kati ya hiyo ameitumikia nchi kwa weledi, umahiri, kujituma, ushujaa, nidhamu na kwa mafanikio ya hali ya juu, akiishi kiapo chake cha kuwa tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya ulinzi wa taifa letu.
“Ametuachia mfano bora wa utumishi wa umma utakaoendelea kuwa mwanga ndani na nje ya majeshi yetu. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi," aliongeza.
HISTORIA YAKE
Mkazi wa Musoma mkoani Mara, aliyejitambulisha kwa jina la John Biseko, aliyekuwa naye mstari wa mbele katika vita vya Tanzania na Uganda mwaka 1978 hadi 1979, alisema Musuguri alizaliwa Januari 4, 1920 Butiama mkoani Mara na kujiunga na jeshi mwaka 1942.
"Kilikuwa ni kipindi cha utawala wa mkoloni, wakati jeshi likiwa chini ya utawala wa Waingereza likiitwa King's African Rifles (KAR). Wakati huo jeshi lilikuwa likifanya kazi nchi tatu za Afrika Mashariki za wakati huo ambazo ni Tanganyika, Kenya na Uganda zikiwa koloni la Uingereza," alisema Biseko.
Alisema mwaka 1947 wakati akiwa na cheo cha Sajini, Musuguri alikuwa miongoni mwa wakufunzi wa KAR, Nairobi nchini Kenya.
Biseko alisema mmoja wa wanafunzi wa Msuguri alikuwa Idi Amin Dada wa Uganda ambaye mwaka 1979 alimtimua katika nchi ya Uganda wakati wa Vita vya Kagera.
"Mimi nilikuwa mmoja wa waliopigana vita ya Uganda, hivyo ninaelewa vizuri ujasiri wa Musuguri. Tulikuwa naye mstari wa mbele na kufanikiwa kumtimua Amin wakati wa vita vya Tanzania na Uganda," alisema.
Pia alisema wakati wa Vita Kuu vya Pili vya Dunia (1939 hadi 1945), Musuguri alipelekwa kupigana Madagascar katika Jeshi la KAR. Baada ya Tanganyika kupata uhuru, jeshi lote la KAR lilihamishiwa katika Jeshi la Tanganyika huru chini ya Waziri Mkuu wa Kwanza, Julius Nyerere likiitwa Tanganyika Rifles.
Biseko alisema jeshi hilo liliundwa mwaka 1961 na kuvunjwa mwaka 1964 na kuanzishwa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambapo mwaka 1962 na Musuguri alipandishwa cheo na kuwa Luteni.
"Wakati jeshi linafanya uasi mwaka 1964, tayari Musuguri alikuwa Tabora katika kambi ya jeshi hilo Brigedia Namba 201. Miaka ya 1970 mwanzoni, Musuguri alipanda cheo na kuwa Brigedia na kuwa Mkuu wa Kikosi Namba 201 na kwamba ndiye aliyeiongoza JWTZ katika uwanja wa mapambano katika Vita vya Uganda.
"Baada ya vita hiyo, Rais Julius Nyerere alimteua kuwa Mkuu wa Majeshi na kutumikia nafasi hiyo kuanzia mwaka 1980 hadi 1988 alipostaafu na kurudi kijijini kwao, Butiama baada ya kulitumikia jeshi kwa miaka 46 na sasa amefariki dunia," alisema.
Wakuu wa majeshi walioongoza tangu kuundwa kwa jeshi hilo hadi sasa na miaka kwenye mabano ni Jenerali Hagai Mirisho Sarakikya (1964 - 1974), Jenerali Abdalah Twalipo (1974 - 1980), Jenerali Musuguri (1980 - 1988), Jenerali Ernest Mwita Kiaro (1988- 1994), Jenerali Robert Mbomav (1994 -2001), Jenerali George Waitara (2001 – 2007), Jenerali Davis Mwamunyange (2007 -2017), Jenerali Venance Mabeyo (2017 – 2022) na Jenerali Jacob Mkunda kuanzia mwaka 2022 hadi sasa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED