Polisi yamaliza utata wa kifo cha mwanafunzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:38 AM Mar 16 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP) Simon Maigwa.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP) Simon Maigwa.

HATIMAYE Jeshi la Polisi, limejitokeza hadharani kumaliza utata kuhusu madai ya kutaka kupotezwa kwa haki za mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Mrupanga iliyoko Uru, wilaya ya Moshi, Janathan Makanyaga (6), anayedaiwa kufariki dunia baada ya kucharazwa bakora na mwalimu wake.

Uchunguzi wa jeshi hilo, umebaini kuwa baada ya mwanafunzi huyo kuadhibiwa, alipelekwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) Februari 28, mwaka huu, bila kutolewa taarifa polisi.

Baada ya kufikishwa hospitalini hapo, inaelezwa Jonathan alifariki dunia Machi 11, mwaka huu wakati akipatiwa matibabu.

Jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP) Simon Maigwa, alisema tayari jeshi hilo linawashikilia walimu watano tarajali, waliokuwa katika mafunzo ya vitendo kwa ajili ya mahojiano.

“Tunawashikilia baada ya kuripotiwa na bibi wa mwanafunzi aitwaye Janathan Stephan Makanyaga (6), mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Mrupanga, kuhusika na kifo cha mwanafunzi huyo.

“Inadaiwa mwanafunzi huyo, aliadhibiwa na walimu hao kwa fimbo Februari 28, 2024 kisha kupelekwa Hospitali ya Rufani ya KCMC bila kutoa taarifa Polisi, na alifariki dunia 11/3/2024 akiwa anapatiwa matibabu hospitalini hapo. Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za kufariki kwa mwanafunzi huyo tarehe 11/3/2024 na kuanza uchunguzi mara moja ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa walimu hao,” alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, mwili wa Jonathan umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.

Alisema uchunguzi kuhusina na tuhuma hizo umekamilika na shauri hilo limepelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), kwa ajili ya kulitolea uamuzi.

Inaelezwa kwamba chanzo cha kuadhibiwa mwanafunzi huyo ni kuchelewa kuwahi kushika namba.

Baadhi ya vyanzo vya taarifa vinaeleza kuwa mwanafunzi huyo alipoingia darasani alianza kutokwa damu puani na mdomoni.

Katika tukio lingine, Polisi inamshikilia mtuhumiwa mmoja (jina limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi) na wengine wanaendelea kutafutwa kwa tuhuma za mauaji ya Hussein Mrutu (19), mkazi wa Mtaa wa Sadini, Kata ya Makuyuni, Moshi.

Kamanda Maigwa alisema mauaji hayo yalitokea Machi Mosi, mwaka huu, na kwamba siku ya tukuio, inadaiwa kulitokea ugomvi kati ya Mrutu na watuhumiwa hao wakiwa wanakunywa pombe katika baa ndogo ya Museveni na kusababisha mauaji hayo.