Mwanafunzi auawa, mwili wakutwa kichakani

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 10:40 AM Apr 14 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda.
PICHA: MAKTABA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda.

MWANAFUNZI wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kilima, wilayani Bukoba, Elius Antony (13), anadaiwa kuuawa kwa kukatwa panga shingoni kisha mwili wake kutelekezwa kichakani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, amesema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.

Akisimulia tukio hilo, mama mzazi wa mtoto huyo, Beatrida Antony, amesema mara ya mwisho kijana huyo alikwenda na baba yake kuchoma mkaa porini, kisha alirudi nyumbani kufuata simu na Sh. 10,000 kwa ajili ya matumizi.

Amesema baba yake aliporejea alipokewa na salamu za pole kutoka kwa majirani kuhusu kupotea kwa mtoto.

“Baada ya muda mfupi alifika Mwenyekiti wa Kijiji na kumchukua baba yake na kumpeleka kichakani ambako mwili huo ulionekana ukiwa umejaa nzi,” amesimulia.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilimo, Izidory Kaiza, amesema Aprili 10, mwaka huu, alipokea taarifa za kupotea kwa mtoto huyo kutoka kwa wazazi wake ndipo ufuatiliaji ukaanza mara moja.

“Wakati tukiendelea kumtafuta tuliona nguo na mguu kichakani katika Kitongoji cha Mwizi na baadaye tukaona mwili mzima, hivyo tukawajulisha polisi ambao walifika na kuubeba kisha wazazi wakaitwa kwenda kuutambua,”amesema.

Amesema ilibainika kuwa mwanafunzi huyo alipigwa na panga shingoni na kuvuja damu hali iliyosababisha umauti.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilima, Reginah Richard, amelaani kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wazazi na walezi kuwa makini kwa kuwalinda  watoto wao.