Mwalimu adaiwa kumbaka mwanafunzi wake

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:15 AM May 10 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Safia Jongo.
Picha: Maktaba
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Safia Jongo.

MWALIMU wa Shule ya Sekondari Katoro (jina linahifadhiwa) miaka36 anadaiwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha tatu alipomtuma nyumbani kwake kisha kumfuata na kumfanyia ukatili huo.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Safia Jongo, huku akibainisha kuwa lilitokea Mei 2, mwaka huu.

Kamanda Jongo amesema siku ya tukio, mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa), alikuwa darasani ndipo mwalimu huto alimwagiza  kwenda nyumbani kwake kumchukulia kitu huku akimfuata kwa nyuma.

Amesema binti huyo alipofika nyumbani kwa mwalimu huyo, alishtuka kuona mlango unafungwa kisha kuanza kufanyiwa ukatili na mwalimu huyo.

SACP Jongo amesema baada ya tukio hilo, mwanafunzi alikwenda kutoa taarifa  kwa mkuu wa shule kwamba mkuu huyo kwa kushirikiana na mtuhumiwa, walimtisha kuwa watamwadhibu kama atatoa taarifa sehemu yoyote. 

“Tulipata tarifa Mei 5 na kuchukua hatua ya kumkatamata mtuhumiwa pamoja na mkuu wa shule na baada ya hapo, utaratibu wa kisheria unaendelea na hatua zaidi zitachukuliwa dhii yao baada ya kukamilisha uchunguzi,” amesema Kamanda Jongo.

Aidha, kamanda huyo amewataka wazazi, walimu na walezi kuwa na tabia ya kuwahoji watoto wanapotoka shuleni ili kama kuna matatizo wanakumbana nayo, wayabaini mapema. 

Katika hatua nyingine, Kamanda Jongo amethibitisha kutokea kwa tukio la mtoto  Kazungu Julius (10) mwenye ualibino na mwanafunzi wa Shule ya Msingi Katoro, kujeruhiwa  kwa kukatwa na mapanga maeneo mbalimbali ya mwili ikiwemo kichwani na mikononi na mtu aliyekuwa amefunika uso wake.

SACP Jongo amesema tukio hilo lilitokea Mei 4, mwaka huu saa 2:00 usiku, wakati mtoto huyo alipotoka nje baada ya kutumwa na mama yake, ndipo alipovamiwa na mtu huyo aliyeanza kumjeruhi kisha kutokomea kusikojulikana.

Amesema kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, tukio hilo ni la kupangwa na wala si la imani za kishirikina za kuhitaji kuondoka na kiungo chochote cha kijana hiyo.

“Mtu huyu tunaendelea kumsaka popote atakapokuwa. Lakini  pia niwatoe hofu wananchi na watu wenye ualibino kuwa na amani kwani kwa mujibu wa daktari, mtu huyo hakuwa na nia ya kuondoka na kiungo chochote kutokana na majereha pamoja na aina ya panga lililokutwa eneo la tukio,” amesema Kamanda Jongo.