MKUU wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Calvin Koola, amesema kuna viongozi wa kanisa wamejigeuza kuwa trafiki ibadani, wakati wa huduma ya matoleo.
Kutokana na kutopendezwa na ujanja huo wa baadhi ya viongozi wa kanisa, alisema jukumu lao si kukwepa kutoa sadaka kama wengine, bali ni kusimamia matoleo.
Mch. Koola alikuwa akizungumza katika Usharika wa Mwika, wakati wa mkutano mkuu wa tatu wa usharika huo unaoongozwa na Mchungaji Godlisten Terry.
Alisema viongozi hao wanachopaswa kukifanya, ni kuwa mfano mwema wa kumtumikia Mungu, wakati wa matoleo ya sadaka, kwa kuwa hivi sasa wako ambao hawatoi sadaka.
Katika mafundisho yake, aliwakemea viongozi mbalimbali katika sharika, ambao siyo mfano mwema wa utoaji kwani wao huwa kama ‘matrafiki ibadani’, ambao kazi yao ni kuwaelekeza washarika kupita huku au kule wakati wa matoleo.
“Wao wenyewe hawatoi sadaka. Ni muhimu wazee wa usharika wawe mfano mwema wa kumtumikia Mungu kwa sadaka. Isivyo bahati, wale wanaomtumikia Mungu kwa uaminifu hukumbana na vipingamizi vingi kutoka kwa kina Sambalati na Thobia; ambao wamejaa dharau na kubeza kazi inayofanywa na wale waliojitoa kwa dhati kumtegemea na kumtumikia Mungu.
“Ni muhimu usharika unapoweka mipango ya maendeleo na kuazimia kuitekeleza katika mkutano mkuu, washarika wasikatishwe tamaa kwa maneno ya dharau na kebehi kama vile hata hiki wanachokijenga, mbwa akipanda ataangusha ukuta.
“Washarika watiwe moyo kwamba, hata kama ni wanyonge, kujaribu ni bora kuliko kutokujaribu au kukata tamaa. Ni lazima tufanye uamuzi kwamba, kazi hii tuliyopewa na Mungu itafanyika. Niwatahadharishe wajumbe wa mkutano mkuu wasiwe ni watu wa kulala katika vikao na kisha kukurupuka na kusema ipite,” alisema.
Akiwasilisha Mpango Mkakati wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT wa mwaka 2024- 2028, Mratibu wa Makavazi ya Dayosisi hiyo, Mch. Enock Makundi, alisema mkutano huo mkuu wa tatu wa usharika, unapaswa kuazimia kuwa na mpango kazi wa usharika unaojielekeza katika mpango mkakati huo wenye vipaumbele vitano.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED